Dodoma. Shirika la Posta Tanzania limepanga kuanza kuwatumia wataalamu wa lugha ya alama kuwezesha mawasiliano baina ya watoa huduma na watu wenye changamoto ya kusikia (viziwi) wanaofika vituoni kupata huduma.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Shirika hilo kutoka Dodoma, Dongwe Dongwe wakati akizungumza na wataalamu wa anuai za jamii kutoka Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Akizungumza na wataalamu hao jijini Dodoma leo Ijumaa Februari 2025, Dongwe amesema lengo la matumizi ya wataalamu hao ni kuondoa adha ya kutokuelewana baina ya watoa huduma na wenye changamoto hizo pindi wanapofika vituoni.
Dongwe amesema katika kipindi hiki wamekuwa wakilazimika kutumia njia ya maandishi kama nyezo ya kuwasiliana na wateja wa aina hiyo kitu ambacho si salama kwa kuwa, huweza kumnyima mteja uhuru wa kutoa baadhi ya taarifa zake, hivyo kukwamisha utoaji wa baadhi ya huduma kwa wateja.
“Yupo mteja mmoja aliwahi kuja ana matatizo ya kusikia ikabidi tuwasiliane kwa kuandika ili kumpatia huduma aliyokuwa anahitaji, lakini kwa sasa tumepanga kuimarisha matumizi ya lugha ya alama kwa watu hao katika utoaji wa huduma kwa ajili ya watu hao,” amesema Dongwe.
Ameongeza kuwa, matumizi ya wataalamu hao yatatanguliwa na utoaji wa mafunzo kuhusu namna ya kuhudumia watu wanaotoka kwenye kundi hilo na makundi mengine yanaowiana ikiwamo watoto, wazee na wanawake.
Mkurugenzi msaidizi wa anuai za jamii kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mwanaamani Mtoro amesema kuwa Serikali imepanga kufikisha huduma hizo kwa watoto ili kuwajengea uwezo wa matumizi sahihi ya teknolojia kuanzia wakiwa wadogo.
Mwanaamani amesema lengo la huduma hiyo ni kuwajengea watoto uwezo wa matumizi ya teknolojia wakiwa na umri mdogo na kuwakinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Ameeleza kuwa, huduma hizo zitatolewa kupitia vituo vya utoaji huduma jumuishi vilivyopo chini ya Posta na taasisi za elimu kwa kuweka mazingira wezeshi ikiwamo vifaa vya kiteknolojia na wataalamu.
“Wizara imepanga kupeleka huduma za kidijitali kwa watoto ili kuwalinda na matumizi mabaya ya teknolojia kwa kuwapa elimu kuanzia wakiwa wadogo na kuwajengea uwezo wa matumizi sahihi ya teknolojia kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesema Mwanaamani.
Mshauri mwelekezi wa makundi anuai, Caroline Ndosi ametoa wito kwa shirika hilo kuweka vifaa vya kidijitali ikiwamo vifaa vya usikivu, programu maalumu kwenye kompyuta ili kuimarisha haki ya faragha na ulinzi wa taarifa za watu hao wanapokwenda kupatiwa huduma.