Ukeketaji ukipungua, wadau wataka sheria kulinda wanawake watu wazima

Dar es Salaam. Wakati matukio ya ukeketaji yakitajwa kupungua hadi kufikia asilimia nane, wadau wa haki za binadamu wameitaka Serikali kutunga sheria maalum ya kupinga ukeketaji itakayowalinda pia wanawake watu wazima.

Pia, wametaka kutungwa na kutekelezwa kwa sheria ndogo-ndogo katika mikoa yenye viwango vikubwa vya matukio ya ukeketaji, sambamba na kufanyiwa marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, hususan kuhusu umri wa ndoa kwa mtoto.

Maoni hayo yametolewa leo Ijumaa, Februari 6, 2026, ikiwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji inayoadhimishwa kwa kauli mbiu isemayo, “Sauti yetu; tokomeza ukeketaji.”

Wadau hao, wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, wamesema utekelezaji wa mapendekezo hayo utasaidia kupunguza zaidi au kutokomeza kabisa matukio ya ukeketaji nchini.

Aidha, wamepongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau, ambazo zimechangia kupungua kwa matukio hayo, ikiwemo maboresho ya sheria, yakiwamo marekebisho ya Sheria ya Mtoto na Kanuni ya Adhabu, pamoja na utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.

Akizungumza katika mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL), Joshua Ntandu, amesema licha ya kupungua kwa matukio ya ukatili huo, bado baadhi ya mikoa inaendelea kuongoza kwa viwango vya ukeketaji.

Ntandu amesema utafiti wa Demografia na Afya Tanzania wa mwaka 2022 unaonyesha kuwa Mkoa wa Arusha ulirekodi ongezeko la matukio ya ukeketaji hadi kufikia asilimia 43 kutoka asilimia 41 mwaka 2015/2016.

Ameongeza kuwa mikoa mingine iliyoripoti viwango vikubwa ni Manyara (asilimia 43), Mara (asilimia 28), Singida (asilimia 20), Tanga (asilimia 19) na Dodoma (asilimia 18).

Amesema sababu za baadhi ya mikoa kuendelea kuongoza na mingine kuibuka katika takwimu ni pamoja na muingiliano wa jamii unaotokana na uhamaji wa watu kutoka maeneo mbalimbali.

Hata hivyo, imebainika kuwa nyuma ya ukatili huo kumeibuka biashara haramu ya viungo vinavyotokana na ukeketaji. Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na Mwananchi umeonyesha kuwa biashara hiyo inaongeza ugumu wa kutokomeza mila hiyo potofu, licha ya kuwapo sera, sheria na kanuni zinazoipiga marufuku.

Uchunguzi huo uliofanyika katika wilaya za Butiama, Tarime na Serengeti mkoani Mara, umebaini kuwa imani za kishirikina ndizo huchochea biashara hiyo ya siri inayohusisha uuzaji wa sehemu nyeti za wanawake zilizokatwa.

Katika ufuatiliaji huo, imeelezwa kuwa baadhi ya viongozi wa kimila na ngariba wanahusishwa na biashara hiyo, ikiaminiwa kuwa wamiliki wa boti za uvuvi huzitumia katika shughuli zao na kujilinda dhidi ya mikosi.

“Ongezeko la matukio haya katika baadhi ya mikoa na mingine kuibuka kwenye takwimu ni ishara ya hatari ya kusambaa kwa ukeketaji kimya kimya endapo juhudi hazitaimarishwa,” amesema Ntandu, huku akisisitiza kuwa utungaji na utekelezaji wa sheria ndogo-ndogo katika mikoa yenye viwango vikubwa utaendelea kupunguza matukio hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, amesema kuna haja ya kutungwa kwa sheria maalum ya kupinga ukeketaji itakayolinda pia wanawake watu wazima, akieleza kuwa bado wapo wanawake wa umri mkubwa wanaofanyiwa ukatili huo.

Amesisitiza umuhimu wa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria zilizopo na kuwawajibisha wote wanaohusika.

“Ili kutokomeza matukio haya, ni muhimu kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo,” amesema Henga.

Aidha, ameitaka Serikali kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya kitaifa na kikanda, ikiwemo kukabiliana na ukeketaji unaovuka mipaka, huku akisisitiza uwajibikaji wa wazazi, walezi na viongozi wa mila wanaohusika na vitendo hivyo.

Naye, Mkurugenzi wa taasisi ya kutetea haki za watoto ya Green Kids and Youth Foundation, Vaileth Mwazembe, ameshauri kuongezwa kwa rasilimali na programu za ulinzi kwa wasichana walio katika hatari, pamoja na kutoa elimu mbadala na msaada wa kijamii na kiuchumi kwa jamii zinazoendelea kushikilia mila hiyo.