Arusha. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kaskazini, limeteketeza bidhaa mbalimbali zenye uzito wa tani tatu zilizokuwa zimekwisha muda wa matumizi pamoja na zilizopigwa marufuku kutumika nchini kutokana na kuwa na viambata vinavyohatarisha afya ya binadamu.
Uteketezaji wa bidhaa hizo umefanyika leo Ijumaa, Februari 6, 2026 katika Jalala Kuu la Jiji la Arusha lililopo Kata ya Murieti. Tukio hilo lilishuhudiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacobo Julius Rombo, pamoja na Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira wa Jiji la Arusha, James Lobikoki.
Akizungumza katika tukio hilo, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini, Edward Mwamilawa amesema bidhaa hizo ziliondolewa sokoni baada ya shirika hilo kufanya oparesheni mbalimbali na kubaini kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu au zimepigwa marufuku kuingizwa nchini kwa mujibu wa sheria.
Amesema miongoni mwa bidhaa zilizoteketezwa ni vipodozi vilivyokuwa na viambata vya sumu ambavyo haviruhusiwi kuingizwa nchini kwa matumizi ya binadamu, huku vingine vikibainika kuuzwa sokoni kwa njia za kificho.
“Katika oparesheni mbalimbali tulibaini uwepo wa vipodozi vyenye viambata hatarishi ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu. Tuliviondoa sokoni na leo tunaviteketeza. “Pia, tulikuta bidhaa za maziwa ya watoto wachanga ambazo hazijasajiliwa na TBS, hivyo tumeziondoa ili kuhakikisha soko letu linakuwa na bidhaa salama,” amesema Mwamilawa.
Ameongeza kuwa, kundi lingine la bidhaa zilizoteketezwa ni nguo za ndani za mitumba, sidiria na soksi, ambazo kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia usalama wa afya za watumiaji haziruhusiwi kuingizwa wala kuuzwa nchini.
Amesema kulikuwapo pia na bidhaa za vyakula zilizokuwa zimekwisha muda wake wa matumizi.
Mwamilawa amesema bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi mara nyingi huuzwa na wafanyabiashara wasio waaminifu, ambao huendelea kuzisambaza sokoni bila kujali madhara yanayoweza kuwapata walaji.
“Hali hii inaweza kuhatarisha afya za wananchi. TBS hatuwezi kukaa kimya kwa kuwa jukumu letu ni kulinda afya za walaji, ambao kimsingi ni Watanzania wote,” amesema.
Amesema ukamataji wa bidhaa zisizo na sifa ni zoezi endelevu katika mikoa yote ya Kanda ya Kaskazini inayojumuisha Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Amewataka waagizaji wa bidhaa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Viwango ya mwaka 2009 kwa kuingiza bidhaa zinazokubalika kisheria na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa bidhaa zao, hususan vyakula, ili kubaini mapema kuisha kwa muda wa matumizi.
Ameongeza kuwa baadhi ya waagizaji wana uelewa wa bidhaa zilizopigwa marufuku kuingizwa na kuuzwa nchini, lakini bado huendelea kufanya hivyo kwa makusudi, hasa kwa vipodozi na kuviuza kwa njia za siri.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacobo Julius Rombo, amepongeza hatua iliyochukuliwa na TBS, akisema inalenga kulinda afya na usalama wa wananchi. Amewataka wananchi kuwa waangalifu na kuhakikisha wanatumia bidhaa salama na zenye ithibati halali kutoka kwa mamlaka husika.