WAHITIMU WA MASTERS, CHUO CHA UHASIBU ARUSHA WATAKIWA KUFANYIA TAFITI CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI JAMII

Na Seif Mangwangi, Michuzi TV Arusha

SERIKALI imewataka wahitimu wa Shahada ya uzamili katika chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kujiimarisha katika tafiti mbalimbali za kitaaluma na kutoa majibu ya changamoto halisi zinazoikabili Taifa katika masuala ya usimamizi wa fedha, ukuaji wa uchumi jumuishi, ajira,ubunifu na matumizi sahihi ya teknolojia.

Wito huo umetolewa leo 6 Februari 2026 na Waziri wa fedha Balozi Khamisi Omar Mussa katika hotuba yake wakati wa mahafali ya ishirini na saba (27), duru ya pili kwa wahitimu wa Shahada ya uzamili(Masters), katika chuo cha Uhasibu Arusha.

“Katika nchi yoyote yenye dhamira ya maendeleo ya kweli kama ilivyo kwa nchi yetu ya Tanzania, Utafiti na Maendeleo ni nyenzo muhimu katika kuongeza ubunifu, kutatua changamoto, kuongeza tija katika uzalishaji na kutoa mwongozo katika uundaji wa sera mbalimbali hivyo. Tasnifu zenu ziwe chachu ya sera bora, maamuzi sahihi na maendeleo endelevu kwa wananchi na Taifa letu,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu, ikiwemo IAA, ili mitaala iendelee kuendana na mahitaji halisi ya soko la ajira na mabadiliko ya uchumi wa kidijitali.

Mkuu wa chuo hicho Profesa Eliamani Sedoyeka amesema Chuo cha Uhasibu Arusha inajivunia kuwa miongoni mwa taasisi za elimu ya juu nchini zinazotekeleza mwelekeo wa Kitaifa wa kupanua upatikanaji wa elimu ya juu kwa kuanzisha na kuimarisha mfumo jumuishi wa utoaji wa shahada ya Uzamili (Master’s degree) unaochanganya masomo ya ana kwa ana darasani (Physical classes) na ya mtandaoni kwa wakati mmoja yaani ‘blended mode’.

“Mfumo huu unaendana kikamilifu na sera za taifa za matumizi ya TEHAMA katika elimu, na umewezesha wataalam walioko katika maeneo mbalimbali ya nchini kuendelea na masomo bila kuathiri majukumu yao ya kazi na huduma kwa jamii,”amesema.

Amesema kupitia mfumo huo bunifu, Chuo kimeongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya Uzamili, kuboresha ubora wa ujifunzaji, na kuendana na mabadiliko ya dunia ya kazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Profesa Sedoyeka amesema Chuo kimeweka mkakati mahususi wa kuwawezesha wahadhiri wengi zaidi kusomea Shahada ya Uzamivu ndani na nje ya nchi, ili kukidhi ongezeko la idadi ya wanafunzi wa Uzamili linaloendelea kushuhudiwa kila mwaka.

“Katika mwaka wa masomo 2025/2026 jumla ya wahadhiri 115 wamepelekwa kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi. Mkakati huu unalenga kuhakikisha uwiano sahihi kati ya wanafunzi na wahadhiri, kuimarisha usimamizi wa tafiti, na kuongeza uwezo wa Chuo katika uzalishaji wa wataalam wanaokidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa,” amesema.

Aidha amesema jumla ya wahitimu waliohitimu shahada za uzamili katika mahafali hayo ni 2,250 kati yao wanaume ni 1,369 sawa na asilimia 60.8 na wanawake ni 881 sawa na asilimia 39.2 .

Profesa Sedoyeka amesema IAA imeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi binafsi na taasisi za umma ndani na nje ya nchi, lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya msingi ya kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.

Amesema ushirikiano huo umewezesha wanafunzi wa chuo hicho kushiriki katika tafiti shirikishi, makongamano, na miradi mbalimbali yenye mchango mkubwa katika kutatua changamoto halisi za kijamii na kiuchumi.

“Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na vyombo vya ulinzi ambavyo ni Jeshi la Polisi kupitia Shule ya Polisi Tanzania (TPS) na Jeshi la Magereza kupitia Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA),” amesema na kuongeza:

“Ushirikiano huu ni umezaa matunda ambayo leo katika mahafali haya miongoni mwa wahitimu tunashuhudia Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza wapatao tisini (90) na Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi mia kumi na moja (111) ambao wanahitimu kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo chetu,” amesema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza la chuo Dkt. Mwamini Tulli amesema katika mahafali ya 27 Duru ya kwanza iliyofanyika tarehe 19 Disemba 2025 kulikuwa na jumla ya Wahitimu 4895 kati yao wanaume walikuwa 2858 na wanawake 2037 ambao walitunukiwa vyeti katika ngazi tatu tofauti ambazo ni Shahada, Stashahada na Astashahada/Cheti.