……………
Na Sixmund Begashe, Ruvuma
Wahitimu wa Mafunzo ya Uhifadhi na Utalii wametakiwa kuzingatia utoaji wa huduma bora inayozingatia ukarimu kwa wageni ili kuvutia wageni wengi na kuongeza mchango katika pato ka Taifa unaotokana na sekta ya Utalii na uhifadhi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Utalii, Bw. Nkoba Mabula ameyasema hayo wakati wa Mahafali ya Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi Maliasili kwa Jamii – Likuyu
Bw. Mabula amesema kuwa, kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuinua Utalii nchini, imeiwezesha sekta hiyo kuchangia asilimia 21 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni na kutoa fursa ya ajira kwa takribani asilimia 11 ya ajira zote hapa nchini na hivyo jitihada hizo zinapaswa kuungwa mkono.
Amewataka wahitimu hao kutumia ujuzi na mafunzo waliyoyapata kuwawezesha kuchangamkia fursa mbalimbali za ajira zinazotolewa na Serikali ili wakawe miongoni mwa wataalamu wanaoleta tija nchini.
Aidha, amekipongeza Chuo hicho kwa kuendelea kuwa nguzo muhimu kwa wizara ya maliasili na utalii kwa kutoa elimu ya uhifadhi wa Maliasili uliojikita kwa Jamii hususan mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS).
” Nitoe wito kwa mashirika ya uhifadhi TANAPA, TAWA, TFS pamoja na wadau wengine wa uhifadhi na Utalii kuendelea kuwatumia vijana hawa kwenye utendaji kazi kwani wana ujuzi na weledi wa kutosha katika kuendeleza Uhifadhi na Utalii” . Alisema Bw. Mabula
Naye Mkuu wa Chuo hicho Bi Jane Nyau amesema kwa mwaka wa masomo 2024/2025 jumla ya wanafunzi mia moja kumi na tatu (115) wa kozi ya Utalii na Uongozaji Watalii wakiwemo 64 wa ngazi ya Astashahada na 51 wa ngazi ya Stashahada wamefanikiwa kuhitimu mafunzo yao leo.
“Leo pia tutahitimisha mafunzo ya kozi Na. 78/2025 yenye jumla ya Askari Wanyamapori wa Vijiji 25 yaliyofanyika kwa muda wa miezi mitatu (3)”. Aliongeza Bi. Nyau.
Mahafali hayo yanehudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo Dkt. Edward Kohi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi SAC. Fidelis Kapala, viongozi wengine wa Menejimenti ya Wizara hiyo, viongozi mbambali na wananchi



