SERIKALI imeomba msaada wa China katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ili kuhakikisha Tanzania iko tayari kuandaa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kushirikiana na majirani zake wa Afrika Mashariki.
Ombi hilo limetolewa jana Ijumaa, Februari 6, 2026 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Millya, wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kichina yaliyofanyika katika Ubalozi wa China jijini Dar es Salaam.
Millya amesema maandalizi ya Afcon 2027 hayahusu soka pekee, bali ni fursa ya kimkakati kwa Tanzania katika kuchochea mabadiliko ya kiuchumi, kupanua miundombinu na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kwa Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Amebainisha kuwa, kuandaa mashindano hayo kutahitaji uwekezaji mkubwa katika viwanja vya michezo vinavyokidhi viwango vya kimataifa, mifumo bora ya usafiri pamoja na miundombinu ya kijamii inayosaidia.
“Kwa kuzingatia ushirikiano wa muda mrefu na wa karibu uliopo kati ya Tanzania na China, tunaomba msaada endelevu wa China ili kuhakikisha miundombinu muhimu kwa AFCON 2027 inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa kimataifa,” amesema.
Ameongeza kuwa, mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia uwekezaji, kutoa ajira, kuboresha miundombinu ya taifa na kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa kama kivutio kikuu cha utalii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Msimamizi wa Masuala ya Ubalozi wa China nchini Tanzania, Wang Yong, amesema maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kichina yanaashiria mshikamano na safari ya pamoja ya maendeleo kati ya China na Tanzania.
Amesema China inaingia katika Mwaka wa Farasi, unaoashiria ujasiri, nguvu na maendeleo.
Wang amesema China inaendelea kupiga hatua za kiuchumi, kisiasa na kijamii chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping, sambamba na kupanua mchango wake katika utawala wa kimataifa na maendeleo endelevu.
Amethibitisha kuwa uhusiano wa China na Tanzania umejengwa juu ya urafiki wa kihistoria na ushirikiano wa vitendo, akitaja miradi mikubwa ya miundombinu ikiwamo ukarabati wa reli ya TAZARA, unaofadhiliwa kwa msaada wa kifedha, kitaalamu na kiusimamizi kutoka China.
“Raia wa China waliopo Tanzania wakiwamo wafanyakazi, walimu, wanafunzi na wafanyabiashara wana mchango mkubwa katika kuhamasisha uhamishaji wa ujuzi, ushirikiano wa kiuchumi na kubadilishana maarifa,” amesema Wang.
Juni 19, 2027 hadi Julai 18, 2027, Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON 2027 kwa kushirikiana na Uganda na Kenya.
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kuandaa mashindano makubwa ya CAF baada ya Agosti 2, 2025 hadi Agosti 30, 2025 kuandaa CHAN 2024 kwa ushirikiano pia wa Kenya na Uganda.