RAUNDI ya 17 ya lala salama ya Ligi ya Championship inaendelea tena Jumamosi hii kwa mechi tatu kupigwa kwenye viwanja mbalimbali na nyingine zikiendelea Jumapili, huku kila timu ikipambana kwa ajili ya kujitengenezea nafasi nzuri.
Kwenye Uwanja wa Filbert Bayi, Kibaha mkoani Pwani, wenyeji maafande wa Transit Camp waliochapwa mabao 2-1, dhidi ya Kagera Sugar katika mechi iliyopita, wana kibarua cha kupambana na vinara wa Ligi, Geita Gold iliyoichapa Barberian FC bao 1-0.
Geita inayoongoza ikiwa na pointi 40, inakutana na Transit Camp iliyo nafasi ya nne kwa pointi 33, ambapo mara ya mwisho kukutana ilikuwa ni raundi ya pili msimu huu na kushuhudia zikitoka sare ya bao 1-1, kwenye Uwanja wa Nyankumbu Geita.
Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025 wa Championship ilimaliza katika nafasi ya nne kwa pointi 56, ikinolewa na aliyekuwa kocha mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.
Geita ilicheza mtoano ili kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu kwa pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare ya 2-2 nyumbani, kisha kuchapwa 2-0 ugenini.
Mechi nyingine itapigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ambapo Gunners FC yenye kumbukumbu ya kushinda mabao 2-1, dhidi ya KenGold, itaikaribisha Songea United iliyotoka kuchapwa bao 1-0 na kikosi cha Stand United ‘Chama la Wana’.
Gunners inashika nafasi ya 12 kwa pointi 17, baada ya kushinda mechi nne, sare tano na kupoteza saba, huku kwa upande wa Songea United ikiwa ya nane kwa pointi 21, ambapo mara ya mwisho timu hizo kukutana zilitoka sare ya kufungana bao 1-1.
Mechi ya mwisho kwa leo Jumamosi itapigwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, ambako Stand United ‘Chama la Wana’, iliyoichapa Songea United bao 1-0, itaikaribisha KenGold ya Mbeya yenye kumbukumbu ya kuchapwa 2-1 na Gunners FC.
Stand United ‘Chama la Wana’, ilishuka daraja msimu wa 2018-2019, ikimaliza katika nafasi ya 19 kwa pointi 44, baada ya kikosi hicho chenye maskani yake Shinyanga, kushinda mechi 12, sare nane na kupoteza 18, kikifunga mabao 38 na kuruhusu 50.
Msimu uliopita, Stand ilimaliza ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 61, ambapo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara, ikianza kwa kuiondosha Geita Gold iliyomaliza ya nne kwa pointi 56, katika Ligi ya Championship kwa jumla ya mabao 4-2.
Baada ya Stand kuitoa Geita Gold, ikacheza ‘Play-Offs’ nyingine dhidi ya Fountain Gate iliyotolewa pia hatua hiyo na maafande wa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo kikosi hicho kilikwama kupanda baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-1.
Ligi hiyo itaendelea tena Jumapili hii kwa mechi tatu pia kupigwa, ambapo Bigman iliyolazimishwa suluhu (0-0), dhidi ya TMA ya jijini Arusha, itakuwa kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi kucheza na Mbuni FC iliyochapwa na Mbeya Kwanza mabao 2-0.
Hausung FC baada ya kuichapa African Sports ya Tanga mabao 2-1, itaendelea kubakia kwenye Uwanja wa Amani uliopo Mkoa wa Njombe kuwakaribisha maafande wa Polisi Tanzania, wenye kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na kikosi cha B19 FC.
Polisi msimu uliopita wa 2024-2025, haukuwa mzuri sana baada ya kumaliza katika nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship kwa pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, ambapo safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza katika nafasi ya 15 kwa pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
Mechi ya mwisho ya raundi ya 17, itapigwa kwenye Kituo cha Ufundi cha TFF, Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambapo B19 FC iliyotoka sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania, itaikaribisha African Sports ya Tanga iliyochapwa na Hausung FC mabao 2-1.
Akizungumzia mwenendo wa Championship hadi sasa, Kocha wa Gunners, Mathias Wandiba, alisema raundi ya pili ni ngumu sana kutokana na mahitaji na malengo ya kila timu, ingawa kuanza vyema majukumu yake mapya ni jambo jema katika kikosi hicho.
“Ligi ina makundi matatu yenye malengo tofauti, la kwanza ni zinazopambania nafasi nne za juu, la pili ni zinazopigania kubakia na la mwisho ni lile la kuepuka mchujo wa kushuka daraja, hivyo, ni lazima tujipange sana,” alisema Wandiba.