Lindi. Watu wawili wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Kampuni ya Maning Nice lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, baada ya kugonga lori lililokuwa limeharibika eneo la Mtange, Manispaa ya Lindi.
Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi Februari 7, 2026, saa 12 asubuhi na kusababisha vifo vya watu hao wawili akiwamo mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Akizungumza na waandishi wa habari, muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Yusuph Salim amesema hospitali hiyo imepokea miili miwili pamoja na majeruhi 12 majira ya saa 1:15 asubuhi.
Amesema kati ya majeruhi hao, wawili wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi, huku 10 wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
“Tumepokea miili miwili, mmoja ni mwanaume mwenye umri wa miaka 50 na mwingine ni mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
“Miili hiyo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hapa hospitalini, majeruhi 10 wanaendelea na matibabu na wawili wakipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili,” amesema Salim.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Rajabu Masoud mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam, amewataka madereva wa vyombo vya usafiri kushirikiana katika kuendesha magari wanaposafiri ili kupunguza ajali barabarani.
Amesema wakati basi hilo lilipofika Lindi, alimsikia dereva akimwomba dereva mwenzake ampokee kuendesha watakapofika eneo la Mnazi Mmoja, hata hivyo hawakufanikiwa kufika eneo hilo, ajali ikatokea.
“Nawaomba madereva wanaposafiri wasaidiane kuendesha ili kupunguza ajali. Pia, wanaoharibikiwa na magari njiani wajitahidi kuweka alama za tahadhari kuanzia mbali ili kuwaonya watumiaji wengine wa barabara,” amesema Masoud.