Wahandisi watakiwa kutekeleza maono ya Serikali kilimo cha umwagiliaji

Iringa. Wahandisi nchini wametakiwa kutekeleza kwa vitendo maono ya Serikali katika maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji kwa kufanya kazi kwa weledi, uzalendo na uwajibikaji ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaleta tija kwa wakulima na kuchangia usalama wa chakula nchini.

Akizungumza jana Februari 6, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Royal Palm, Manispaa ya Iringa, wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka wahandisi kutekeleza majukumu yao kwa kujituma na kulinda maslahi ya taifa katika miradi yote ya umwagiliaji.

Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoanza Februari 2–6, 2026 yalihusisha mada za usimamizi wa mikataba, sheria ya ununuzi pamoja na utafiti wa miamba katika mabwawa.

“Nisisitize na kusema kuwa miradi ya umwagiliaji inahitaji dhamira ya dhati na uaminifu kwa nchi,” amesema RC James.

RC James amesema wahandisi wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kutekeleza maono ya Rais, Waziri na Mkurugenzi wa Umwagiliaji kuhusu kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini.

“Ijulikane kuwa mafanikio ya sekta hii ya kilimo cha umwagiliaji yanategemea sana namna majukumu yanavyotekelezwa,” amesema RC James.

Vilevile, RC James amewakumbusha washiriki kuwa kila mpango wa maendeleo una muda maalumu wa utekelezaji, hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanazingatia ratiba na kutimiza majukumu waliyopewa kwa wakati.

RC James amewataka watumishi kutumia maarifa waliyopata katika mafunzo hayo kuboresha uzalishaji wa kilimo cha umwagiliaji, akisema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika ustawi wa wananchi na uchumi wa taifa.

“Na Serikali ina imani kubwa na wahandisi wake na inatarajia kuona matokeo chanya yatokanayo na mafunzo hayo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umwagiliaji,” amesema RC James.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amesema tume imejipanga kuhakikisha mafunzo hayo yanatoa matokeo chanya kwa maendeleo ya sekta hiyo.

Katika hatua nyingine, Mndolwa ameahidi kuwa watumishi wa tume watafanya kazi kwa uadilifu na kujituma.

“Na uongozi wa tume utaendelea kusimamia miradi ya umwagiliaji kwa karibu ili kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na kuleta manufaa kwa wakulima,” amesema Mndolwa.

Mndolwa amesisitiza kuwa tume inaendelea na ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji pamoja na juhudi za kuvuna na kuhifadhi maji kwa matumizi ya kilimo katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika kulinda mazingira, Mndolwa amesema tume imekuwa ikitekeleza shughuli za upandaji miti katika maeneo ya miradi ya umwagiliaji na kuwa jitihada hizo zinalenga kulinda vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo ambao ni wahandisi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kutoka mikoa yote nchini wamesema kuwa wamepata uelewa mpana kuhusu majukumu yao na umuhimu wa kuyatekeleza kwa umakini mkubwa.

Wahandisi hao wamesema kuwa kupitia mafunzo hayo wamejifunza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu katika utekelezaji wa miradi ili kuepuka changamoto zisizo za lazima.

“Mafunzo haya ya siku tano yametuwezesha kutujengea uelewa juu ya utafiti wa miamba,” amesema Meneja wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) Mkoa wa Iringa, Peter Akonaay, huku akiongeza kuwa:

“Pia yametujengea uelewa wa Sheria ya Manunuzi na usimamizi wa mikataba na yatatusaidia kusimamia ubora wa miradi ili kufanikisha malengo ya Serikali kuwa na miradi endelevu.”

Baadhi ya wahandisi wameeleza kuwa utafiti wa miamba katika mabwawa ni hatua muhimu inayohitaji umakini mkubwa kabla ya utekelezaji wa miradi.