Meli ya kwanza ya EACOP kusafirisha mafuta Julai

Dar es Salaam. Tanzania na Uganda zimepiga hatua mpya katika kuimarisha diplomasia ya kiuchumi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kuwa meli ya kwanza ya kusafirisha mafuta ghafi kupitia Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) inatarajiwa kuondoka Bandari ya Chongoleani, Tanga, mwezi Julai mwaka huu.

Rais Samia amesema hayo leo Jumamosi, Februari 7, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

“Mradi wa EACOP umefikia hatua nzuri na mwezi Julai mwaka huu tunatarajia kuona meli ya kwanza ikisafirisha mafuta kutoka Bandari ya Chongoleani, jambo ambalo ni fahari kwa Tanzania na Uganda,” amesema Rais Samia.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la kimkakati la nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku ukiwa chachu ya ongezeko la mapato ya Serikali, ajira na fursa za uwekezaji kwa wananchi.

Katika mazungumzo hayo, Rais Samia amesema Tanzania iko tayari kumuunga mkono Rais Museveni katika juhudi za kuimarisha amani na usalama katika ukanda wa Maziwa Makuu, akitaja nafasi yake kama mwenyekiti wa jumuiya hiyo kuwa muhimu katika kuleta uthabiti wa kikanda.

“Rais Museveni kwa sasa ni mwenyekiti wa nchi za Maziwa Makuu na ana mkakati wa kuanzisha mazungumzo ya kuleta usalama ndani ya ukanda huo. Tanzania tumemwambia tunamuunga mkono na tuko tayari kumsaidia atakavyoona inafaa,” amesema Rais Samia.

Amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kikamilifu na nchi wanachama wa Maziwa Makuu katika kuhakikisha kunakuwepo na utulivu wa kudumu, akibainisha kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amesema umefika wakati kwa mataifa ya Afrika kujiimarisha kiusalama na kujihami bila kuacha hatima ya bara hilo iamuliwe na mataifa ya nje.

Amesema Afrika ina uwezo wa kujisimamia kikamilifu endapo itatumia vyema rasilimali zake na kuimarisha mshikamano wa kidiplomasia na kiuchumi.

Rais Museveni amesema kwa muda mrefu mataifa ya Afrika yamekuwa yakikosa mikakati madhubuti ya kujilinda dhidi ya ushawishi na vitisho kutoka nje, hali iliyochangia kuyumbisha uwezo wa nchi hizo kufanya maamuzi huru kwa masilahi yao.

“Hatuna sababu ya kuogopa mataifa ya nje kuamua mustakabali wetu ilhali tuna rasilimali za kutosha na uwezo wa kujisimamia. Tunachohitaji ni umoja na dhamira ya pamoja,” amesema Rais Museveni.

Ameongeza kuwa umoja wa Afrika ndio njia sahihi ya kulinda masilahi ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi ya bara hilo katika dunia ya ushindani wa kimataifa.