::::::::::
WAKAZI wa Kijiji cha Mwangaza Kata ya Kasenga wilayani Chato mkoani Geita, wameonyesha kufurahishwa na ujenzi wa daraja lenye historia ya kusababisha vifo vya wananchi watatu.
Wametoa pongezi zao mbele ya mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Peter Bura, aliyetembelea eneo hilo katika ziara ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye Kata ya Kasenga, Katende, Muungano na Chato.
Awali akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwangaza, Bura amepokea pongezi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye Kata hiyo na kwamba jamii hiyo inaona mwanga mpya wa maendeleo.
“Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa kuamua kutujengea daraja hili ambalo lilisha sababisha vifo vya watu watatu, kabla ya ujenzi wake kufikia hatua hii wazazi wengi walikuwa wanakuja hapa kupokea watoto wao wakati wa kutoka shule ili kuwavusha”,
“Eneo hili kipindi cha mvua lilikuwa likikata mawasiliano ya wananchi kuvuka upande mmoja kwenda mwingine, lakini kwa sasa kama mnavyoona Tarura wamefanya kazi kubwa sana kunusuru maisha ya wananchi wetu, ispokuwa tunaomba ikiwezekana barabara hii iende hadi Mwangaza sentani” amesema Samwel Mganga.
Akizungumzia ujenzi wa daraja hilo, Meneja wa Wakala wa barabara za vijijini na mijini (Tarura) Mhandisi Ernest Nyanda, amesema ujenzi huo umegharimu kiasi cha Tsh. 123,431,780 na kwamba umefikia aslimia 98.
Mbali na daraja hilo, jumla ya km 3 za barabara zimechongwa kutoka Mwangaza hadi Butacha hali iliyorahisisha usafirishaji mazao ya wakulima na shughuli zingine za kibinadamu.
Hata hivyo, ameonyesha kusikitishwa na baadhi ya wafugaji kudhoofisha jitihada za serikali kwa kupitisha mifugo yao kwenye barabara hiyo, hali inayosababisha kuharibika na kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.
Kutokana na hali hiyo, Bura akalazimika kutoa kauli ya serikali kwa viongozi wa Chama na serikali waliopo kwenye Kata ya Kasenga kuhakikisha wanakuwa walinzi na wasimamizi wa miundo mbinu hiyo kwa maslahi mapana ya umma.
Amesema serikali inatumia fedha nyingi kutekekeza ujenzi wa barabara na madaraja, hivyo ipo haja kwa viongozi kutafuta njia bora ya kuzuia mifugo kupitia kwenye barabara hiyo ili iweze kudumu na kuwanufaisha wananchi wengi.
Kauli ya mkuu wa wilaya hiyo, inaungwa mkono wa msemo wa wahenga usemao “Kitunze kudumu” wakimaanisha ukihifadhi kwa wivu mkubwa na kukifanyia ukarabati kile kilicho katika himaya yako ili kisipoteze uthamani wake.
Mwisho.


