Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kufanya uteuzi wa viongozi na kuongeza vitengo katika baadhi ya wizara, wachambuzi na wachumi wamekuwa na mitazamo tofauti.
Baadhi wanasema mabadiliko hayo yanabeba mageuzi ya namna Serikali inavyotekeleza majukumu yake, kusimamia rasilimali na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi huku wengine wakidai itaongeza mzigo katika utendaji.
Wameyasema hayo ikiwa ni baada ya Rais Samia kufanya mabadiliko ya muundo wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Wizara ya Nishati kwa kuzifanya kuwa na Makatibu Wakuu wawili kwa kila wizara.
Aidha, katika mabadiliko ya muundo huo, pia amewateua Dk Tausi Kida kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, huku Dk Fred Msemwa akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Uwekezaji.
Taarifa ya mabadiliko hayo, ilitolewa jana Ijumaa Februari 6, 2026 na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, akimrejea Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.
Katika taarifa hiyo, Dk James Mataragio ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati anayeshughulikia (mafuta na gesi asilia), huku Felchesmi Mramba akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati anayeshughulikia (umeme na nishati jadidifu).
Katika upande mwingine, Rais Samia amemteua Sosthenes Kewe kuwa Naibu Katibu Mtendaji, Tume ya Taifa ya Mipango anayeshughulikia ufuatiliaji na tathmini, akichukua nafasi ya Dk Linda Ezekiel ambaye atapangiwa majukumu mengine.
Akizungumzia mabadiliko hayo, mchambuzi wa masuala ya uchumi, Dk Lutengano Mwinuka amesema uwepo wa vitengo hivyo utasaidia wao kufanya kazi katika namna inayotakiwa katika maeneo ya kisekta.
Dk Mwinuka amesema hatua hiyo itachangia pia upatikanaji wa taarifa sahihi pale inapohitajika ufafanuzi ikiwa ni bungeni au kwa wananchi.
“Miundo inabadilika kila siku na kuleta taswira ya ukubwa wa majukumu yaliyopo, mtu akiwa na majukumu mengi anashindwa kuyatekeleza kwa ufanisi unaotakiwa.
“Kuweka watu watakaokuwa na jukumu la kufanya kazi katika maeneo mahususi, inasaidia kuonekana kwa matokeo tarajiwa,” amesema Dk Mwinuka.
Maelezo yake yaliungwa mkono na Dk Felix Nandonde wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), aliyesema katika jicho la kawaida, uteuzi huo unaweza kuonekana kama unaongeza gharama kwa Serikali, lakini utaongeza ufanisi kwa kiasi kikubwa.
Dk Nandonde amesema kuongeza vitengo wakati mwingine huchochewa na mabadiliko yanayotokea ndani ya wizara yanayoendana na uelekeo wa nchi, jambo linaloonyesha uhitaji wa uwepo wa mtu anayeweza kulisimamia ipasavyo.
Ametolea mfano wa Wizara ya Nishati kwamba atakayesimamia umeme na nishati jadidifu atakuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kuendana na mipango ya nchi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 katika kupeleka umeme kwenye maeneo ya vijijini.
“Ndugu aliyepewa hapo ana kazi ya kwenda kufanya, ndani yake atakuwa na taasisi kadhaa. Kwenye nishati jadidifu pia tunaona Katibu Mkuu atakwenda kufanya kazi ya ziada.
“Katika mipango ya muda mrefu ni moja ya njia ya kupunguza majukumu kwa watendaji ili wasiwe na majukumu makubwa,” amesema Dk Nandonde.
Amefafanua kuwa mtu mmoja kusimamia wizara nzima kama Katibu Mkuu, angeweza kupwaya katika baadhi ya maeneo na kuweka nguvu zaidi katika maeneo ambayo ana ufanisi nayo.
“Kuweka mtu mmoja itawezesha kufikia mafanikio. Kwenye gesi amewekwa Dk Mataragio ni mtaalamu, ataisaidia nchi kufikia malengo yake ya uzalishaji gesi huko Lindi na Mtwara,” amesema.
“Kama uteuzi ulifanyika kwa kuangalia namna ya kuongeza ufanisi na uwajibikaji, basi hii inaweza kuwa na tija kama watendaji wataenda kufanya kazi kwa umakini mkubwa, tutaona mabadiliko ndani ya muda mfupi,” amesema.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Said Miraji amesema alichokifanya Rais Samia ni kuonyesha uzito na namna gani amekusudia kusimamia utendaji kazi.
Miraji amesema Rais Samia asingeweza kutengeneza wizara nzima kama wizara ya tiba, wizara ya afya, wizara ya vifaa tiba lakini kuzipa nguvu za kiutendaji ndiyo ameamua kuweka makatibu wakuu.
“Unajua Waziri anasimamia masuala ya sera, anaweza kuwa anasimamia utekelezaji wa dira, ilani za uchaguzi, anajikita katika masuala ya siasa lakini Katibu Mkuu anajikita zaidi katika utendaji,” amesema.
Alitolea mfano suala la gesi akisema zamani ilikuwa ikichukuliwa kama kitu ambacho si cha muhimu sana, lakini sasa ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa nchi na maisha ya watu.
Katika upande wa nishati jadidifu, Miraji amesema ni vyema imetambuliwa kama sekta, awali haikupewa kipaumbele cha kutosha huku akitolea mfano mkazo unaowekwa katika matumizi ya umeme jua, lakini bado vifaa vinavyotegemewa ni kutoka nje.
“Mtu wa kijijini akiambiwa aweke sola anahitaji hadi Sh5 milioni kwa ajili ya kuwezesha umeme kuwaka kwake na akisema aweke vifaa vya umeme vinavyoweza kuendeshwa na umeme huo ni gharama kubwa na havipo vya kutosha, mtu anaona kwa nini usisubiri umeme wa REA (Wakala wa Umeme Vijijini) akaweka kwa Sh150,000,” amesema.
Amesema katika mtazamo wa jumla, uteuzi huu utakwenda kuongeza nguvu ya utendaji kutafuta mawazo zaidi, kutafuta uwajibikaji zaidi, kuongeza ubunifu zaidi, usimamizi na utekelezaji wa miradi kwa haraka zaidi kuliko awali mtu.
Mchambuzi wa siasa, Dk Richard Mbunda amesema katika kipindi kama hiki ni kuongeza huduma za uendeshaji na huenda kukawa hakuna faida.
“Katika kipindi ambacho kikapu kimepungukiwa, wahisani hawatoi fedha bila kujulikana hali hii itakuwa kwa muda gani sidhani kama ni sahihi kuendelea kugawa wizara.
“Nilidhani ni kipindi ambacho tulipaswa kupunguza gharama. Wizara sijui ziko ngapi zingepunguzwa badala ya kuendelea kuongeza mawaziri, makatibu wakuu,” amesema Dk Mbunda.
Dk Mbunda amesema hali hiyo ni kama kuongeza mzigo katika kipindi ambacho nchi haijafanya vizuri zaidi kiuchumi na katika ukusanyaji wa mapato kwa kiwango kilichotakiwa.
Hata hivyo, mabadiliko ya muundo wa wizara hiyo na uteuzi wote kwa ujumla alioufanya Rais huenda ukaenda kuongeza joto la uteuzi mwingine katika nafasi mbalimbali zikiwamo za ukurugenzi wa halmashauri au manispaa, ukatibu tawala wa mkoa, ukatibu mkuu wa wizara na ukuu wa mkoa na wilaya.
Taarifa ambazo Mwananchi inazo zinadai kuelekea miezi michache ijayo kuna baadhi ya watendaji wa nyadhifa mbalimbali wanakwenda kustaafu baada ya muda wao wa kuhudumu kutamatika kwa mujibu wa sheria.
Kama hiyo haitoshi, taarifa hizo zinadai kuna baadhi ya vigogo waliopo katika maeneo mbalimbali wamekuwa chini ‘sio active’ kama awali, kutokana na kuhofia mkeka wa mabadiliko ambao haujajulikana utatolewa lini na mkuu huyo wa nchi.
Kauli ya Spika wa Bunge, Mussa Zungu kuhusu utendaji wa Serikali hasa suala la mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri na majibu ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, yanachagiza zaidi joto la mabadiliko katika nafasi za watendaji mbalimbali.
Jana Ijumaa Februari 7, 2026 katika Mkutano wa pili wa Bunge la 13, Zungu aliibua changamoto kuhusu utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri, akisema uwezo wa baadhi ya benki katika mitaji ya ukopeshaji umekuwa kikwazo kikuu cha walengwa kutofikiwa kwa wakati.
Katika majibu yake, Dk Mwigulu alitoa tamko akieleza kupunguzwa kwa masharti ya mikopo hiyo, akisema hivi sasa kigezo kikubwa kitakuwa ni Kitambulisho cha Taifa (Nida).
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wabunge kuhakikisha wanawafuata wananchi waliko na kuzungumza nao moja kwa moja ili kusikiliza kero zinazowakabili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kanali Yahya Kido ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera akichukua nafasi ya Fatma Mwassa na Kanali Donald Msengi ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, akichukua nafasi ya Kanali Patrick Sawala atakayepangiwa majukumu mengine.
Aidha, Rais Samia amemteua Balozi Waziri Salum kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, akichukua nafasi ya Dk Hashil Abdallah ambaye atapangiwa majukumu mengine.
Uteuzi huo pia, umehusisha makatibu tawala wa mikoa, Dk Toba Nguvila ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, akichukua nafasi ya Missaile Musa ambaye amestaafu.
Dk Stephen Nindi ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, akichukua nafasi ya Judica Omary ambaye amestaafu.
Kwa upande wa manaibu Katibu Wakuu, Nsubili Joshua ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha anayeshughulikia huduma za hazina.
Joshua anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenifa Omolo ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana.
Aristides Mbwasi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, akichukua nafasi ya Dk Suleiman Serera ambaye atapangiwa majukumu mengine.
Profesa Mohammed Sheikh ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia masuala ya uvuvi, huku Dk Edwin Mhede aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo atapangiwa majukumu mengine.
Rose Ambrose ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Emmanuel Tayari ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya dawa na vifaa tiba.
Profesa Peter Msoffe amehamishwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya mazao na usalama wa chakula, akichukua nafasi ya Dk Stephen Nindi ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe;
Dk Fabian Madele ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia masuala ya mifugo na Balozi Barak Luvanda ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya mazingira.
Pia, Meja Jenerali Marco Gaguti ameteuliwa kuwa Balozi na atapangiwa kituo na Dk Hassan Mshinda ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).