RAIS SAMIA APONGEZWA KWA KUPUNGUZA UHABA WA WATUMISHI HANDENI MJI

Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Handeni, Amiri Mwaliko,akizungumza katika mkutano wa kupokea na kujadili taarifa za kata za Halmashauri ya Mji Handeni uliofanyika leo Februari 7, 2026.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju,akizungumza katika mkutano wa kupokea na kujadili taarifa za kata za Halmashauri ya Mji Handeni uliofanyika leo Februari 7, 2026.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Reuben Kwagilwa,akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese,wakati wa  mkutano wa kupokea na kujadili taarifa za kata za Halmashauri ya Mji Handeni uliofanyika leo Februari 7, 2026.

Sehemu ya Madiwani wakifuatilia mkutano wa kupokea na kujadili taarifa za kata za Halmashauri ya Mji Handeni uliofanyika leo Februari 7, 2026.

Na Augusta Njoji

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Mji Handeni, Mhe. Amiri Mwaliko, amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali cha ajira kilichowezesha kupatikana kwa watumishi 82 wa kada mbalimbali na hivyo kupunguza uhaba wa watumishi katika halmashauri hiyo.

Akifungua mkutano wa kupokea na kujadili taarifa za kata wa Halmashauri hiyo uliofanyika Februari 7, 2026 mjini hapa, Mhe. Mwaliko amesema serikali imeendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi.

“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kutatua changamoto ya watumishi. Tunafurahia hatua hii kwa kuwa lengo la serikali ni kuondoa uhaba wa watumishi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema.

Aidha, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, kwa kuhakikisha wilaya hiyo inaendelea kudumisha amani na utulivu.

Mhe. Mwaliko amewataka viongozi na watumishi kushirikiana katika kujenga halmashauri yenye mshikamano na kutatua changamoto zinazojitokeza.

Ameongeza kuwa ni muhimu kusimama pamoja na watumishi na kushughulikia changamoto kwa njia ya mazungumzo ili kujenga timu imara ya utendaji kwa maendeleo ya halmashauri.

Kadhalika, amesisitiza kuendelea kuchukuliwa hatua za kudhibiti utoro wa wanafunzi kwa kushirikiana na madiwani wa maeneo husika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 serikali imeajiri watumishi 82 wakiwemo walimu wa shule za msingi na sekondari pamoja na wauguzi.

Amesema changamoto ya upungufu wa watumishi inaendelea kupatiwa ufumbuzi kadri serikali inavyoendelea kutoa ajira, huku halmashauri ikiendelea kutenga bajeti kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya kata, ikiwemo ununuzi wa madawati.