Serikali imewataka vijana wanaopata fursa za ajira nje ya nchi kuwa mabalozi wa Taifa kwa kuzingatia nidhamu, uadilifu na tamaduni katika nchi wanazokwenda, ili kulinda heshima ya Tanzania.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo, leo Februari 07, 2026 katika ukumbi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaaga rasmi vijana 200 wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kisuo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi ya kusimamia ajira nje ya nchi, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata ajira zenye staha.
Ameeleza kuwa, Serikali imeendelea kuratibu na kusimamia shughuli za Mawakala Binafsi wa Ajira waliosajiliwa, ambao wanauganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira, Jane Sorogo, amewashukuru Mawakala Binafsi wa Ajira kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali katika kuwaandaa vijana wanaopata fursa za ajira nje ya nchi.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Mawakala wa Ajira nchini, Rashid Milao, ametoa wito kwa vijana waliopata fursa hizo za ajira kuzingatia maelekezo wanaliyopewa na Serikali ili kuiwakilisha vyema Tanzania kimataifa.
