UNICEF yawapa wasanii jukumu la kupambana na ukatili

Kwa muda mrefu, tasnia ya muziki imekuwa ikilaumiwa kwa kuzalisha nyimbo zenye maudhui yanayodaiwa kukinzana na maadili ya jamii. Hali hiyo imekuja wakati jamii ikiendelea kukabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, masuala ambayo wengi wanaona hayajapewa uzito unaostahili kupitia kazi za sanaa.

Hata hivyo hoja hiyo pia iliwekwa wazi katika mjadala ulioandaliwa na UNICEF kwa kushirikiana na Sauti za Busara, uliojikita katika namna wasanii wanavyoweza kutumia sauti na ushawishi wao kukemea ukatili na kutetea haki za wanawake na watoto.

Mjadala huo uliwakutanisha wasanii, wadau wa sanaa na wataalamu wa ulinzi wa watoto, kwa lengo la kuhimiza utengenezaji wa maudhui yatakazoishi vizazi na vizazi.

 Akizungumza katika mjadala huo Februari 6,2026, Balozi wa Vijana wa UNICEF Nabiha Kassim alisema kizazi cha Gen Z mara nyingi huvutiwa kwanza na mdundo kabla ya kuzingatia maneno ya wimbo, jambo linalowalazimu wasanii kuzingatia ubora wa beat sambamba na ujumbe.

“Kuandaa wimbo unaokemea ukatili wa watoto hakumaanishi wimbo huo uwe mbaya au usiovutia,” alisema. “Inawezekana kabisa kuwa na wimbo mzuri, unaochezeka na unaobeba ujumbe mzito yote yanategemea ubunifu wa msanii.”

Aliongeza kuwa wasanii wanapaswa kutambua utofauti wa hadhira yao. “Wengi hulenga makundi fulani, lakini wanapaswa pia kubeba hisia za jamii nzima. Wakati wengine wakisherehekea, wapo wanaoumia na muziki unaweza kuzungumza na pande zote.”

Kwa upande wake, msanii wa singeli Man Fongo alisema mjadala huo umempa msukumo mpya wa mwelekeo wa kazi zake. Alisema amejipanga kuandaa nyimbo zitakazotetea haki za wanawake na watoto na kupinga vitendo vya ukatili.

“Nitatumia muziki mzuri kuwafikishia watu ujumbe. Wasanii tuna nafasi ya kuelimisha jamii kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia nyimbo zinazopendwa na wengi.”

Aliongeza kuwa maudhui atakayoyazalisha yatazungumzia masuala yanayogusa rika lake na vizazi vilivyotangulia. Huku yakilenga pia kufikia hadhira pana na kuwa na mvuto katika majukwaa ya kidijitali.

Mpenzi wa muziki Jumanne Abdallah alisema mabadiliko hayaanzii kwenye maneno au video pekee, bali kwenye mtazamo na dhamira ya msanii.

“Msanii akiamini kweli kwamba mtoto ana thamani na kwamba kila mtu ni sawa, inakuwa rahisi zaidi kuwasilisha ujumbe. Msanii anaweza kuimba bila kulenga kundi maalum muziki mzuri hufika kila mahali,”alisema

Akichangia kwa mtazamo wa kitaalamu, mtaalamu wa ulinzi wa watoto Ahmed Rashid alisema kuna haja ya kuongeza nyimbo zenye maadili chanya katika kazi za sanaa.

“Tunahitaji muziki unaohamasisha maadili na unaokemea waziwazi ukatili na unyanyasaji wa watoto.Ujumbe huo una nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko.”

Aliongeza kuwa wasanii ni vioo vya jamii. Jamii huiga kile wanachosikia na kukiona kutoka kwa wasanii wao.

Msanii kutoka Kenya Labdi alisema mjadala huo umekuwa fursa muhimu ya kutafakari upya wajibu wa wasanii.

“Wasanii wengi hutengeneza muziki bila kuelewa kikamilifu mahitaji ya kizazi kijacho,” alisema, akibainisha kuwa nchini Kenya kuna mabadiliko yanayoonekana ambapo wasanii wengi wameanza kuandika nyimbo zinazogusa masuala ya unyanyasaji wa watoto na uwajibikaji wa kijamii.

Akihitimisha mjadala huo, Mkuu wa Ulinzi wa Watoto wa UNICEF Miranda Armstrong alisema wasanii wana jukumu kubwa la kusukuma mbele ujumbe unaolinda haki za watoto.

“UNICEF imefanya kazi na mabalozi wengi wa haki za watoto, na wasanii wamekuwa sehemu ya safari hiyo. Tunasubiri kuona wasanii wengi zaidi wakijitokeza kuwa mabalozi wa vijana na watetezi wa haki za watoto.”

Kwa ujumla, mjadala huo uliweka wazi jambo moja muhimu zaidi ya burudani, muziki ni chombo chenye nguvu ya kuunda maadili ya jamii na wasanii wana nafasi ya kipekee kutumia sauti zao si tu kuiburudisha jamii, bali pia kulinda mustakabali wake