Azam yashinda mechi tatu mfululizo CAF

BAADA ya kuanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa vichapo viwili mfululizo, Azam FC imeamka na sasa inatembeza dozi tu kwa wapinzani.

Chini ya Kocha Florent Ibenge, Azam leo Februari 7, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, imeibuka na ushindi wa bao 1-0.

Beki wa kushoto wa Azam, Pascal Msindo ndiye aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 24 akitumia vizuri pasi ya Abdul Suleiman Sopu.

Ushindi huo ni wa tatu mfululizo kwa Azam baada ya kuichapa Nairobi United kwao 2-1, kisha nyumbani 1-0 na leo ikishinda 1-0 nyumbani dhidi ya Maniema. Kabla ya hapo, ilifungwa nyumbani 1-0 na Wydad, kisha kichapo cha 2-0 ugenini kwa Maniema.

Ilikuwa mechi ya lazima Azam kushida huku ikishuhudiwa Aishi Manula kwa mara ya kwanza akidaka kimataifa tangu arejee kikosini hapo msimu huu akitokea Simba.

Licha ya ushindi huo, lakini Azam bado ina kazi ya kufanya ili kufuzu robo fainali, kutokana na sasa kuendelea kukamata nafasi ya tatu kundi B ikifikisha pointi tisa sawa na AS Maniema iliyopo nafasi ya pili na Wydad inayoongoza.

Azam ipo nafasi ya tatu nyuma ya Maniema na Wydad kutokana na kanuni ya ‘head to head’ kwani licha ya leo kuifunga Maniema, lakini tofauti ya mabao imewahukumu kutokana na ugenini kufungwa 2-0, lakini pia ilifungwa 1-0 na Wydad nyumbani. Bado hazijarudiana.

Kesho Jumapili, Wydad itakuwa ugenini kucheza dhidi ya vibonde wa kundi hilo, Nairobi United ambayo haina pointi. Ushindi kwa Wydad kesho utaifanya ikaribie zaidi kufuzu robo fainali ikisubiriwa matokeo ya mechi za mwisho wikiendi ijayo

Azam ina njia mbili za kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, ya kwanza ni kuifunga Wydad nyumbani kwao kwa tofauti ya mabao 2-0 ili kumaliza juu yao kwa kanuni ya ‘head to head’ kwani mechi ya kwanza nyumbani ilifungwa 1-0.

Njia ya pili, kuiombea Maniema mechi ya mwisho ipoteze nyumbani dhidi ya Nairobi United iliyochakazwa mechi zote nne hadi sasa iwe nyumbani au ugenini, kisha yenyewe Azam iambulie hata sare kw Wydad.

Njia zote hizo zinaonekana kuwa ngumu, lakini katika mchezo wa mpira wa miguu, hakuna kinachoshindikana.