Geita. Imepita miezi sita tangu kutoweka kwa Padri Peter Rwezahura wa Shirika la Wamisionari wa Clara, aliyekuwa akihudumu katika Kituo cha Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma.
Kanisa hilo limewaomba Watanzania na watu wa ukanda wa Afrika Mashariki kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 5, 2026 na Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Clara Kanda ya Afrika Mashariki, Padri Joy Mampilikunnel kutoka Makao Makuu ya Shirika Nairobi, Kenya, shirika hilo limeamua kutoa taarifa kwa umma kuhusu kupotea kwa padri huyo, baada ya juhudi zote za awali kushindikana.
“Tungependa kuwajulisha kwa heshima kwamba mmoja wa mapadri mwenzetu, Padri Peter Rwezahura, raia wa Tanzania aliyekuwa akihudumu katika Shule ya Msingi ya Mtakatifu Bakhita, Kituo cha Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma amepotea kwa kipindi cha miezi sita iliyopita. Tumefanya kila juhudi kumtafuta ikiwamo kuomba msaada wa polisi, lakini hadi sasa hatujafanikiwa kumpata,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kupotea kwa padri huyo kumethibitishwa pia na Padri Abel Mwarabu wa Parokia ya Michungwani jijini Dar es Salaam, ambaye amesema lengo la barua hiyo ni kuomba msaada kwa watu kama kuna yeyote mwenye taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa kiongozi huyo wa kiroho.
Padri Mwarabu amesema hali ya kutokuwepo kwa Padri Rwezahura katika eneo lake la kazi na kutopatikana kupitia mawasiliano ya simu kwa muda mrefu, ndicho kilichotafsiriwa kama kapotea.
“Unaposhindwa kumpata mtu kwenye eneo lake la kazi na pia hapatikani kwenye mawasiliano, hali hiyo hutafsiriwa kama kupotea. Ndiyo maana tumeamua kuomba msaada wa jamii wa kumpata,” amesema Padri Mwarabu.
Amesema kama kuna mtu ana taarifa zake au hata kama yeye mwenyewe atapata taarifa kwamba anatafutwa, ajitokeze katika mamlaka husika au kwa viongozi wa shirika.
Mwananchi imezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo kwa simu juu ya taarifa hizo, amethibitisha kupokea taarifa za kupotea kwa padri huyo.
Kamanda Lutumo amesema padri huyo alikuwa akihudumu kama msimamizi wa Shule ya Msingi ya Mtakatifu Bakhita na kabla ya kutoweka, alikuwa amepata uhamisho wa kurejea makao makuu ya shirika hilo mjini Nairobi.
Kamanda Lutumo amesema uchunguzi wa awali umebaini Padri Rwezahura alirejea nyumbani kwao Bukoba kujiandaa kabla ya kwenda Nairobi, lakini hakurejea kituoni kufunga mizigo wala kutekeleza uhamisho huo.
“Hali hiyo iliwafanya wenzake waamue kutoa taarifa polisi baada ya kutoonekana kwa muda,” amesema kamanda huyo.
Hata hivyo, amesema uchunguzi wa awali uliofanywa shuleni alikokuwa akifanya kazi, ulibaini kuwepo kwa taarifa za ufujaji wa rasilimali, vifaa na fedha, jambo lililosababisha shirika kuamua kumhamisha na kumrejesha katika makao makuu yake.
“Baada ya taarifa ya kutoweka kwake kuripotiwa, uchunguzi wa polisi ulibaini alionekana baadaye jijini Dar es Salaam, kabla ya kukatika kwa mawasiliano yake na aliwaambia wenzake kwamba simu yake ilikuwa ikifuatiliwa,” amedai Kamanda Lutumo.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na limewataka wananchi wenye taarifa zozote kuhusu mahali alipo Padri Rwezahura, watoe taarifa kwa mamlaka husika au kituo chochote cha polisi, ili kusaidia kupatikana kwake na kuwaondolea hofu na msongo wa mawazo wenzake wanaoendelea kumtafuta.