USIKU wa jana, zimepigwa mechi tatu za CAF zilizohusisha timu za Tanzania ambapo Yanga ilikabiliana na AS FAR Rabat, huku Simba ikicheza dhidi ya Petro Atletico, hizi zilikuwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika zikicheza ugenini, wakati Azam ikaikaribisha AS Maniema kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Zilikuwa mechi za uamuzi kwa Yanga na Azam, wakati Simba ni sehemu ya kukamilisha ratiba na kuboresha kikosi chao kwa ajili ya mashindano mengine kama alivyosema kocha mkuu wa kikosi hicho, Steve Barker.
Kabla ya mechi hizo, Yanga katika kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikuwa na pointi tano sawa na AS FAR Rabat, huku ushindi wa bao 1-0 ilioupata nyumbani mechi ya kwanza, umeifanya kukaa juu kwa mujibu wa kanuni za CAF ambapo timu zikilingana pointi, cha kwanza wanaangalia matokeo ya timu hizo zilipokutana matokeo yalikuwaje. Wakati huohuo, vinara walikuwa Al Ahly wenye pointi nane waliocheza pia jana dhidi ya JS Kabylie waliokuwa mkiani na pointi mbili.
Kwa upande wa Azam, ilikuwa na pointi sita, ikishika nafasi ya tatu kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika, wakati AS Maniema ikikusanya tisa sawa na Wydad iliyokaa kileleni ambayo leo Jumapili ipo Kenya kucheza na vibonde wa kundi hilo, Nairobi United ikiwa haina pointi.
Simba haina nafasi kutokana na kukusanya pointi moja kabla ya jana kucheza dhidi ya Petro Atletico yenye asilimia kubwa ya kufuzu robo fainali kama ilivyo kwa Stade Malien na Esperance.
Wakati jana zikipigwa mechi hizo tatu za wawakilishi wetu, leo Jumapili ni Singida Black Stars ambayo inasaka ushindi dhidi ya CR Belouizdad ambao ni vinara wa kundi C la Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa na pointi tisa.
Singida inashika nafasi ya mwisho katika kundi hilo, lakini ina pointi nne sawa na Stellenbosch, huku AS Otoho ikiwa nazo sita nafasi ya pili.
Hesabu za Singida kufuzu robo fainali zinaweza kuendelea kuwa hai endapo leo itaibuka na ushindi nyumbani pale New Amaan Complex, Zanzibar, kisha mechi ya mwisho kule Afrika Kusini dhidi ya Stellenbosch, iibuke tena na ushindi, iandike rekodi nyingine baada ya sasa kuwa nayo ile ya kushiriki michuano ya CAF kwa mara ya kwanza na kufuzu makundi kama ilivyofanya Namungo msimu wa 2020-2021.
Ukiweka kando matokeo ya jana, kwa msimu huu wawakilishi wetu hao wanne wameipa heshima Tanzania kutokana na kile walichokifanyika katika mashindano hayo ya CAF.
Kabla ya kwenda mbali, tukukumbushe tu kwamba, kuanzia msimu wa 2019-2020, Tanzania ilianza kuingiza timu nne ambapo Simba na Yanga zilishiriki Ligi ya Mabingwa, huku Azam na KMC, lakini hakuna hata moja iliyotinga makundi.
Kuanzia hapo, Tanzania ikawa haikosi timu hatua ya makundi ambapo 2020-2021 tulikuwa na Namungo upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, ikaishia hapo, wakati Simba ikiwa Ligi ya Mabingwa Afrika ilikwenda hadi robo fainali.
Msimu wa 2021-2022, Simba ilikuwa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa, ikaishia robo fainali. Msimu huo, Yanga pia ilishiriki Ligi ya Mabingwa, wakati Azam na Biashara United zikiwa Kombe la Shirikisho na kutolewa mapema.
Simba na Yanga zikafanya kweli msimu wa 2022-2023 kwa kucheza hatua ya makundi na kuvuka hadi robo fainali ambapo Simba ilikwamia hapo upande wa Ligi ya Mabingwa, huku Yanga ikienda fainali ya Kombe la Shirikisho, ikapoteza kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger, matokeo ya jumla yakiwa 2-2. Mechi ya kwanza nyumbani Yanga ilifungwa 2-1, ugenini ikashinda 1-0.
Msimu wa 2023-2024, Yanga na Simba zote ziliishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikawa ni mafanikio makubwa upande wa michuano hiyo kwa Tanzania wawakilishi wake kucheza hatua hiyo.
Simba nayo ikacheza fainali ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2024-2025, ikapoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane wakati watani zao wa jadi, Yanga wakiishia makundi Ligi ya Mabingwa.
Safari hii 2025-2026 ndiyo funga kazi, timu nne zilizoshiriki mashindano ya CAF, zimefuzu makundi huku zikitazamia kuwania kucheza robo fainali. Matokeo ya mechi za jana yamefanya uamuzi.
Hata hivyo, haikuwa kinyonge msimu huu kwani Azam na Singida Black Stars zimeweka rekodi ya kutinga makundi kwa namna yake. Azam ni mara ya kwanza baada ya kujaribu kwa takribani mara kumi katika mashidano ya CAF na kushindwa kufuzu makundi, safari hii imepenya. Singida ni jaribio moja tu, kwani imeshiriki mashindano ya CAF kwa mara ya kwanza na kufuzu makundi.
Yanga na Simba ni wakongwe, kushiriki kwao mashindano ya CAF imekuwa kama kawaida, lakini kucheza makundi, misimu ya karibuni nayo imeanza kuzoeleka huku Simba ikiwa na rekodi ya kucheza robo fainali saba za CAF katika misimu tisa kuanzia 2018-2019, huku mara moja ikitinga fainali Kombe la Shirikisho msimu wa 2024-2025 kama ilivyofanya Yanga 2022-2023.
Msimu huu hatua ya makundi kwa timu za Tanzania, Azam imekuwa timu ya kwanza kupata ushindi uwanja wa ugenini ilipoichapa Nairobi United 2-1, ilikuwa Januari 25, 2026, maboa yakifungwa na Jephte Kitambala na kipa wa Nairobi United, Ernest Mohamed akijifunga akijaribu kuokoa shuti la Himid Mao.
Singida na Yanga, ndiyo timu ambazo hazijapoteza nyumbani kuanzia mtoano hadi sasa hatua ya makundi, huku Simba na Azam zikionja vipigo mara moja hatua ya makundi.
Kwa namna ambavyo wikiendi ijayo tunakwenda kukamilisha hatua ya makundi, tunaweza kusema wawakilishi wetu wamefanya kazi kubwa sana msimu huu.