Anti usinifikirie vibaya, nalazimika kulisema hili ili nipate msaada naomba unistahi. Nina familia bora na mke mwema asiyepaswa kuudhiwa kwa namna yoyote ile, hilo nakiri na kila mtu analijua.
Ila nahisi kuna jambo baya litatokea nisipopata msaada, hivi karibuni mke wangu amebadili msaidizi wa nyumbani baada ya wa awali kuondoka.
Huyu aliyekuja ni kama sumaku ndani ya moyo wangu ninamfikiria muda wote. Anti ninampenda huyu binti ambaye sidhani kama anazidi miaka 25, kiasi nakosa raha kuna kipindi najichelewesha kurudi nyumbani ili nisimuone niulinde utu na moyo wangu.
Mke wangu anafanya biashara husafiri mara kwa mara, natamani nimzuie kusafiri kipindi hiki, maana nikibaki na huyu binti nitaaibika. Naomba ushauri nifanye nini kabla sijaaibika.
Dah! Katika hili ninakuhurumia na ninakupongeza kwa kuwa muwazi kabla hujajidhalilisha. Umefanya jambo sahihi kusema ukweli mapema kabla haujageuka kituko na kuishia kupata maumivu na kuvunja familia yako.
Ukweli wa kwanza kabisa ni huu: hisia zinaweza kumpata mtu yeyote, lakini maamuzi ndiyo humfanya mtu awe mwaminifu au msaliti.
Wewe bado uko upande mzuri kwa sababu unatambua hatari na unatafuta msaada.
Ni muhimu ujue kwamba hali unayoipitia si mapenzi ya kweli, bali ni mchanganyiko wa mazoea, ukaribu wa kila siku, upweke wa muda mfupi na mwili wa kibinadamu kuitikia vishawishi.
Huyo binti yuko karibu, yupo ndani ya nyumba, anakuona kila siku, na mke wako hayupo mara kwa mara. Huo ni mtego wa kawaida sana uliovunja ndoa nyingi bora kama yako.
Ukikaa kimya ukidhani utajizuia peke yako, unajidanganya. Moyo ukishapata nafasi akili hufuata nyuma, ukija kushituka umeshaharibu na huna namna ya kurekebisha.
Ukweli wa pili mchungu ni huu: huwezi kushinda vita hii ukiwa peke yako ndani ya nyumba moja na huyo binti. Kujichelewesha kurudi nyumbani ni ishara kuwa tayari umeelemewa.
Leo unakwepa, kesho utazoea, kesho kutwa utajikuta umevuka mstari. Si kwa sababu wewe ni mbaya, bali kwa sababu mazingira ni mabaya. Ndiyo maana hatua lazima ichukuliwe sasa, si kesho.
Nakushauri mwambie mke wako ukweli kwa hekima na taadhima. Sio lazima useme “nampenda huyo binti”, bali sema ukweli unalenga suluhisho, si kuumiza.
Mwambie kwamba hujisikii salama kimaadili kuendelea kuishi na msaidizi huyo ndani ya nyumba kwa sababu ya hisia zisizokufurahisha, na unataka kulinda ndoa yenu. Mwanamke anayekupenda atakuthamini zaidi kwa uaminifu huo kuliko kugundua kesho kupitia aibu.
“Ninakupenda, nakuheshimu, na sitaki hata chembe ya fedheha iingie kwenye ndoa yetu. Nimegundua hali ya kutokuwa na amani moyoni kuhusu msaidizi wetu, na ningependa tumsaidie apate kazi mahali pengine au tumtafutie mazingira mengine, si kwa kosa lake bali kwa kulinda ndoa yetu.”
Hilo si udhaifu ni uanaume wa kweli. Mwanamume anayeilinda ndoa yake kabla haijaharibika ni jasiri kuliko anayejitetea ikianguka.
Binti huyo ni mdogo, anatafuta riziki, si wajibu wake kubeba udhaifu wako unapaswa kumlinda, kwa kumtoa kwenye mazingira hatarishi.
Usiichezee ndoa nzuri kwa tamaa ya dakika chache. Umebarikiwa kuwa na mke mwema na familia bora. Linda hicho ulicho nacho. Chukua hatua leo. Usingoje moyo uamue kwa niaba yako.
Hakikisha mkeo anakuelewa, maana anaweza kupuuzia kutokana na shida ya kupaya msaidizi, mng’ang’anie mumtafutie kazi mahali pengine.