Madhila ya ndoa za wenza chotara

Canada. Leo, tutaongelea ndoa za  watu wa rangi mbili tofauti maarufu Kiingereza kwa jina la  Interrracial marriages.

Mara nyingi, katika ndoa hizi, watoto na wazazi huwa waathirika wa ama moja kwa moja au vinginevyo.

Kwanza, watoto hujishangaa na kujiuliza “kwanini mimi sifanani na wenzangu?” Wengine huwakabili wazazi wao na kuwauliza.

Wengine, hasa waliozaliwa kwenye jamii ambapo kuwa mweusi ni kama laana, huogopa hata kuwakabili na kuwauliza wazazi wao.

Katika kukua, hasa watoto waliozaliwa na kukulia kwenye nchi za Magharibi ambako asilimia kubwa ni Wazungu, hujikuta kwenye kuchanganyikiwa na mtanziko kiasi cha kukumbwa na kiwewe (trauma) ambayo inaweza kuwasababisha changamoto kwenye afya ya akili na msongo wa mawazo mbali na kukosa kujiamini na kujithamini.

Tutoe mfano wa Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama. Katika kitabu chake cha Dream of My Father:A Strory of Race and Inheritance (1995), yaani Ndoto ya Baba Yangu, Rangi na Urithi, ameeleza mengi ya aliyopitia kama mtoto chotara.

Anaeleza namna rangi yake ilivyogeuka mzigo kiasi cha kuthubutu kuvuta bangi, kubadili jina na kujiita Barry Obby ili kufanana na wenzake, na mengine mengi tu.

Watoto chotara au rangi mbili au watu wa rangi kama waitwavyo huku Amerika ya Kaskazini,  hupambana na maswali ya kuchanganya na kuudhi kama vile kuambiwa “wewe ni mweusi, wewe ni tofauti nasi, una rangi ya chokoleti” na mengineyo.

Mambo haya humuumiza na kumtesa mhusika kiasi cha kujichukia hata kuwachukia wazazi wake mbali na kumchanganya kiasi cha kujifanya si ajichukie tu bali kujikana kama inavyoonyesha kwenye kadhia ya Obama kubadili jina lake ili awe sawa na wenzake.

Mbali na mtoto, ubaguzi humuathiri mwanandoa asiye mzungu. Ubaguzi unaweza kutoka kwa wanafamilia, marafiki, na hata majirani wa mhusika. Ukiachia kwenye ngazi ya kifamilia, ubaguzi pia upo dukani, hospitali, na hata shuleni.

 Hayo hapo juu yanapotekea, husababisha yafuatayo: Mosi, mhusika anaweza kujitafuta na kujitambua na kusonga mbele kwa kujiamini na akapuuzia ubaguzi na adha vinavyomsumbua na kumzunguka.

Watu hawa ni wale wa aina ya Obama. Baada ya kujitambua na kujikubali, Obama alioa mwanamke mweusi ili kujibainisha yeye ni nani.

Maana, siku mkewe, wakati ule mtarajiwa, Michelle aliwahi kukiri kuwa alipomtambulisha Obama kwa wazazi wake, walizoea kumwambia kuwa amewaletea mtarajiwa mwenye majina ya ajabu.

Pili, wapo wanaoshindwa kujitambua na kujikubali kiasi cha kutafuta namna ya kujikomboa na adha na mateso wanayokutana na kupambana nayo kijamii. Wanaweza ama kuoa au kuolewa na wazungu ili kufuta tofauti walizopambana nazo kwenye makuzi yao au kujiondoa kabisa kwenye mazonge waliyopitia.

Kwa wanandoa, wote wawili huwa na changamoto zitokanazo na ubaguzi wa rangi. Kim Willis mama mzungu aliyeolewa na mwanaume mweusi aitwaye Sydney alilalamika kuwa mwanawe alikuwa akibaguliwa kutokana na kuchanganya rangi (Citynews Vancouver, 2020).

 Kim anasema kuwa yeye na mumewe hawakuwahi kuficha ubaguzi kwa watoto wao. Badala yake waliwaelimisha juu ya kadhia hii. Huu ni mfano mmoja kati ya mingi.

Martha Rossignol anaelezea vizuri madhara ya ubaguzi wa rangi kwa wanandoa kwenye kitabu chake cha My Triumph over Prejudice: A Memoir (Ushindi wangu dhidi ya Ubaguzi: Kumbukumbu, 2016) anaelezea vizuri akisema: “Tulipambana na ubaguzi sana. Unakwenda kwenye mgahawa, watu wanasema hawawezi kukuhudumia. Mkitembea pamoja mtaani, ni kama mlikuwa na gonjwa hatari la kuambukiza.”        

Japo Wazungu hujifanya kupinga ubaguzi, ni watu wanaoongelea na kuthamini rangi yao kuliko kitu chochote. Japo si wote, wengi wao, hasa wale wenye elimu ya kati au wasioelimika kabisa, huongelea rangi mara nyingi kuliko mambo mengine. 

Kwa uzoefu na utafiti wetu utokanao na kuchangia sana kwenye masuala ya ndoa na uhusiano,  majirani zetu ambao ni wakulima huongelea sana rangi mara nyingi.

Kutokana na ufinyu wa nafasi, leo, tungependa tuishie hapa tukiahidi kudurusu na kuwaletea mengi kuhusiana na ndoa mchanganyiko,  uhusiano na malezi ya watoto katika ndoa hizi. Tunaamini itasaidia wanaotaka kuingia kwenye ndoa hizi.