Dar es Salaam. Mamia ya wafanyabiashara na wananchi wamejitokeza kushuhudia ufunguzi wa Soko la Kariakoo, lililokuwa katika ukarabati tangu mwaka 2022 kufuatia ajali ya moto iliyotokea miaka mitano iliyopita na kuteketeza mali zote zilizokuwemo ndani ya soko hilo.
Ufunguzi huo umefanyika leo Februari 8, 2026, katika soko hilo, ambapo pamoja na wafanyabiashara na wananchi, viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa wamehudhuria.
Baada ya ajali hiyo, Serikali ilitoa Sh28 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa soko hilo.
Kati ya fedha hizo, sehemu ilitumika kujenga soko dogo jipya lenye ghorofa sita.
Ukarabati wa soko kuu umehusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kudhibiti majanga ya moto, miundombinu rafiki kwa watu wenye mahitaji maalumu pamoja na uwekaji wa lifti kwa ajili ya kubeba watu na mizigo, hali inayolifanya Soko la Kariakoo kuwa la kisasa zaidi.
Katika kipindi chote cha ukarabati, wafanyabiashara zaidi ya 1,500 waliokuwa wakifanya shughuli zao katika soko hilo walihamishiwa kwa muda katika masoko ya Kisutu, Machinga Complex na Karume.
Hadi sasa, zaidi ya asilimia 80 ya wafanyabiashara hao wamerejeshwa sokoni kwa kupatiwa vizimba na maduka