BAADA ya Coastal Union kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa Februari 6, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, imemfanya kocha mkuu wa timu hiyo, Mohamed Muya, kushinda moja tu kati ya 10 alizoiongoza msimu huu.
Kocha huyo aliyezifundisha Fountain Gate na Geita Gold, alijiunga na Coastal Union, Oktoba 6, 2025, akichukua nafasi ya Alli Mohammed Ameir, aliyeondoka Oktoba 1, 2025. Tangu amechukua mikoba hiyo mambo yamekuwa ni magumu pia kwake.
Tangu Oktoba 6, 2025, Muya ameiongoza Coastal Union katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo ameshinda moja kwa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, Novemba 26, 2025, huku akitoa sare tano na kuchapwa nne.
Katika mechi hizo 10, Coastal Union imefunga mabao matano tu chini ya Muya na kuruhusu 11, ambapo kocha huyo alichukua pia nafasi ya Alli aliyeondoka ikiwa ni muda mfupi baada ya kuchapwa mabao 2-0, dhidi ya Dodoma Jiji, Septemba 27, 2025.
Alli alijiunga na Coastal Union, Agosti 16, 2025, akitokea KVZ FC ya Zanzibar, akisifika kwa uzoefu mkubwa wa kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo, kikosi cha Zanzibar Heroes akiwa kocha msaidizi na kocha mkuu wa vijana Zanzibar.
Msimu wa 2025-2026, Alli aliiongoza Coastal katika mechi tatu za Ligi Kuu, akishinda bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, Septemba 17, 2025, kisha kuchapwa 2-1 na JKT Tanzania Septemba 22, 2025 na 2-0 mbele ya Dodoma Jiji, Septemba 27, 2025.
Wakati huohuo, Kocha Msaidizi wa Coastal Union, Joseph Lazaro amesema benchi la ufundi linashangazwa kwa nini kikosi chao hakifanyi vizuri na kinaendelea kupoteza mechi za Ligi Kuu licha ya kufanya kila kitu kwa usahihi.
Alisema hali hiyo imejenga hofu kwa wachezaji ambao wanaingia kwenye mechi wakiwa hawajiamini jambo ambalo linawafanya wawe na presha.
“Unajua matokeo ya nyuma vilevile yanasababisha timu kufanya vibaya, unawaza leo pia ninaweza kufanya kama jana, kwahiyo hofu imewajaa mpaka wachezaji,” alisema Lazaro.
Alisema wana timu nzuri baada ya kuongezewa nguvu dirisha dogo kwa kuleta wachezaji wazoefu akiwemo Thomas Ulimwengu, James Msuva na wengineo, na mchezo dhidi ya Pamba walitengeneza nafasi nyingi lakini wakafungwa wao.
“Wenzetu walitumia makosa ambayo sisi hatukuyatumia pale walipokosea wao. Sasa ile ari kwamba leo tutafungwa tena kwa kawaida mnajikuta mnapoteza mchezo, lakini siyo kwamba tulicheza vibaya mno, hapana,” alisema Lazaro.
Alisema kikosi chao kinakabiliwa na changamoto ya umaliziaji kwa kutotumia vyema nafasi za mabao zinazotengenezwa na makosa ya kujirudia katika eneo la beki, jambo ambalo linasababishwa na hofu ya kupoteza mechi mara kwa mara.
“Kwahiyo tusipoangalia siyo mechi hizi tu tulizopoteza bali tunaweza kupoteza hata zote, tukae tujiulize kwanini tunapoteza, kwanini tunaruhusu mabao kipindi cha pili kwa sababu tukikufunga goli moja litarudishwa ukitufunga haturudishi,” alisema Lazaro na kuongeza;
“Kwahiyo kwenye uwanja wa mazoezi lazima twende na mentality hiyo wapi tunakosea, je tunachoka. Tusiende kwenye vitu vingine sijui wachezaji au mwalimu mbaya, hapana, tunafungwa wapi tunakosea wapi, na sisemi kama tuna timu mbaya.”
Lazaro alisema pamoja na kuongeza wachezaji wapya wakiwemo wanne katika eneo la ulinzi, bado wanahitaji muda ili wachezaji hao waingie kikosini moja kwa moja huku akiwatoa wasiwasi mashabiki wasikate tamaa.
“Lakini bado hatujakata tama, ni sisi benchi la ufundi kwenda kuangalia kwenye uwanja wa mazoezi kwa sababu hatuna timu mbovu lakini tunafungwa wapi, makosa yako wapi ndicho tutakwenda kufanya,” alisema.