KOCHA msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema changamoto kubwa kwa timu hiyo imekuwa ni kushindwa kumalizia vizuri msimu, licha ya kuanza kwa nguvu kila mwaka.
Simba iko kileleni mwa msimamo na pointi 31 ikiwa ni 11 zaidi na ilizonazo watetezi wa taji la Ligi hiyo, JKT Queens iliyopo nafasi ya tatu yenye nazo 20 imecheza mechi 11 ikishinda 10 na sare moja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mgosi amesema katika misimu ya nyuma Simba Queens imekuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na ubora wa kikosi, lakini hivi karibuni mambo yamekuwa magumu hasa wanapokuwa mwishoni mwa msimu.
Mgosi amesema hilo limekuwa somo kubwa kwa benchi la ufundi msimu huu wanapambana kila mechi watakayocheza wachezaji wajitoe kwa asilimia zote ili kufanikisha malengo yao.
“Kila timu tunayokutana nayo imekuwa ikitupa ushindani mkubwa kwa hiyo kila mechi kwetu ni fainali, misimu ya hivi karibuni tunapoanza huwa inakuwa vizuri kwetu lakini mwishoni inakuwa tofauti,” amesema Mgosi
Kocha huyo aliongeza uamuzi wa kuwaacha wachezaji wengi uliwashtua wengi lakini lengo lilikuwa ni kutengeneza timu mpya na ya muda mrefu ikichanganya wachezaji wachanga.
Aliongeza, kuongoza ligi haina maana kwamba wanapata mechi nyepesi, kwani kila timu inakuja na dhamira ya kuwazuia akisema hilo linawalazimu wachezaji wake kuwa makini zaidi kila wanapoingia uwanjani.