Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila amesema kuanza huduma katika Soko la Kariakoo, jijini Dar es Salaam kutaambatana na kufunguliwa na barabara zote zinazoingia na kutoka sokoni humo.
Hatua hiyo kwa mujibu wa Chalamila, inalenga kuongeza usalama wa soko hilo, urahisi wa huduma na kurahisisha uokozi inapotokea changamoto.
Kauli ya Chalamila inakuja wakati ambao sehemu kubwa ya barabara za kuingia na kutoka sokoni hapo zimefungwa na wafanyabiashara waliopanga biashara zao njiani.
Kutokana na hilo, si gari wala usafiri mwingine unaoweza kupita, kwa sababu ya msongamano wa wafanyabiashara na biashara zao.
Chalamila ameyasema hayo leo, Jumapili Februari 8, 2026 alipotoa salamu za Mkoa wa Dar es Salaam, wakati wa hafla ya uzinduzi wa soko hilo, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema tayari ameshazungumza na wafanyabiashara wote kuanzia sasa barabara zote ndani ya soko hilo zitafunguliwa, ingawa anafahamu maelekezo hayo yanaweza kuwa machungu kwa baadhi ya watu.
“Inawezekana lisiwe jambo zuri na yanaweza kuwa maelekezo machungu kwa wafanyabiashara, lakini huwezi kujenga nyumba yenye thamani ukaziba barabara. Naamini diplomasia itaendelea kutumika pasipo kutumia nguvu kwamba barabara zitabaki wazi,” amesema.
Hatua hiyo, Chalamila amesema itasaidia mji kupumua na kuleta usalama, kadhalika inapotokea dharura itarahisisha utatuzi wa haraka.
“Ufunguaji wa barabara hautakuwa hapa Kariakoo tu. Kila inaponyesha mvua huwa tunafunga barabara, Jangwani, Kariakoo na Kigogo,” amesema.
Sambamba na hilo, amesema katika soko hilo kulikuwa na uhaba wa vyumba na fremu za kufanyia biashara, lakini Rais Samia alielekeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuzindua sera ya ubia itakayokaribisha sekta binafsi kujenga majengo hayo.
Kutokana na hilo, amesema hadi sasa mikataba iliyoingiwa kati ya NHC na sekta binafsi ni zaidi ya 61 kwa ajili ya kubomoa na kujenga upya nyumba hizo.
Chalamila, amesema baada ya hatua hiyo kwa sasa fremu 1,500 za biashara zimezaliwa, nyumba 700 na maeneo mengine yenye thamani ya zaidi ya Sh356 bilioni.
Amesema eneo hilo ni muhimu kikodi, kidiplomasia na kiuchumi na kwa mantiki hiyo lazima kuwe na kila mbinu ya kulilinda ili kodi isizorote.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe amesema ili kuhakikisha soko linatoa huduma kwa ufanisi, Serikali itahakikisha barabara za jirani yake zinafunguliwa ili kuongeza usalama na kuwezesha huduma za saa 24.
Kutokana na uhitaji wa maeneo ya wafanyabiashara wadogo, amesema mpango wa ujenzi wa soko la machinga katika eneo la Bonde la Mto Msimbazi umeanza.
Amesema kwa sasa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili (DMDP II) mkandarasi anatafutwa atakayejenga soko hilo, sambamba na kingo za Mto Msimbazi.