Mohamed Kijuso atangaza vita mpya mapema 

KOCHA msaidizi wa Bigman FC, Mohamed Kijuso, amesema malengo ya timu hiyo kwa sasa ni kumaliza nafasi nne za juu, licha ya ushindani mkubwa uliopo hasa katika mechi za mzunguko wa pili, ambazo ndizo ngumu kutokana na mahitaji ya kila timu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kijuso amesema hadi sasa hawako sehemu mbaya kutokana na pointi ambazo timu hiyo inazo, japo jitihada na umakini vinahitajika, hasa kwa mechi za ugenini ambazo ugumu wake huongezeka mara mbili zaidi ya nyumbani.

“Nafasi ya kumaliza nafasi nne za juu bado ipo kwetu kwa sababu gepu la pointi sio kubwa sana, raundi ya pili huwa ni ngumu kwa kila mechi bila ya kujali mazingira unayocheza, jambo la muhimu ni kucheza kwa umakini sana,” amesema Kijuso.

Kocha huyo wa zamani wa Cosmopolitan, amesema licha ya timu hiyo kutokuwa na balansi nzuri katika eneo la kujilinda na la ushambuliaji, ila kwa sasa anachozingatia ni kikosi hicho kinapata matokeo mazuri bila ya kujali aina ya uchezaji.

Bigman zamani ikifahamika Mwadui, kabla ya mechi ya jana dhidi ya Mbuni, kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya saba na pointi 21, baada ya kushinda mitano, sare sita na kupoteza mitano, huku kikosi hicho kikifunga mabao 13 na kuruhusu 12.