Dar es Salaam. Kuimarisha biashara ndogo na za kati (MSMEs) za wanawake, pamoja na kuwawezesha katika matumizi ya teknolojia za kidijitali, ni miongoni mwa njia muhimu za kuwaendeleza kiuchumi na kuongeza ushindani wao katika soko.
Sambamba na hilo, kuwajengea wanawake ujuzi wa uongozi, kuongeza utayari wao wa kukua kifedha, na kushughulikia vikwazo vya kijamii vinavyokwamisha maendeleo yao ya kiuchumi ni hatua muhimu katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa.
Katika kufanikisha hayo yote, Jukwaa la Wakurugenzi Wakuu Tanzania (CEOrt), kupitia ushirikiano wake na Vodacom, limesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ili kurasimisha ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuharakisha uongozi na ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi hapa nchini.
Ushirikiano huo utatekelezwa kupitia mpango wa CEOrt unaojulikana kama ‘Think Equal, Lead Smart (TELS)’, ulioanzishwa mwaka 2024 kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation, kwa lengo la kukuza usawa wa fursa kwa wanawake katika uongozi, biashara na nafasi za maamuzi.
Kupitia ushirikiano huo, CEOrt na TWCC zitafanya kazi kwa pamoja kuimarisha biashara za wanawake pamoja na kuwajengea ujuzi wa uongozi na biashara.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Benson, amesisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto za kimfumo zinazoendelea kuzuia ushiriki kamili wa wanawake katika masuala ya kiuchumi na uongozi.
“Think Equal, Lead Smart imebuniwa kuunganisha wajasiriamali wanawake na mifumo ya sera, uwekezaji na uongozi. Ushirikiano huu unaimarisha uwezo wetu wa kuwasaidia wanawake wanaojihusisha na shughuli za kiuchumi katika mikoa mbalimbali na kuhakikisha wanawake wanajumuishwa kikamilifu katika mifumo ya maendeleo na uongozi wa Tanzania,” amesema.
Amesema ushirikiano utafungua njia za upatikanaji wa mitaji, masoko na ushauri wa kibiashara kupitia wanachama wa CEOrt na washirika wa kimkakati.
Miunganisho hiyo inatarajiwa kuongeza fursa kwa wanawake kupata mitaji, kuingia katika minyororo ya thamani ya juu zaidi, na kunufaika na mwongozo wa kibiashara pamoja na mitandao ya sekta mbalimbali.
Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, akisisita jambo wakati wa mwendelezo wa mkutano wa program ya Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini ( CEO Roundtable of Tanzania- CEOrt) inayojulikana kama ‘Think Equal, Lead Smart (TELS), ilioanzishwa mwaka 2024 kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation, kwa lengo la kukuza usawa wa fursa kwa wanawake katika uongozi, biashara na nafasi za maamuzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Dk Mwajuma Hamza, amesema ushirikiano huo unashughulikia changamoto halisi zinazowakabili wanawake wajasiriamali nchini.
“Wanachama wetu bado wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mitaji, masoko, ushauri wa kitaalamu na nafasi za maamuzi. Ushirikiano huu na CEOrt unatoa fursa za vitendo kwa wanawake kujenga biashara endelevu, kupata nafasi za uongozi na kushindana kikamilifu katika uchumi,” amesema.
Ushirikiano huo ulitanguliwa na kikao cha kwanza cha maarifa cha Think Equal, Lead Smart, kilichowakutanisha viongozi wa biashara, washirika wa maendeleo, watunga sera na wanawake wajasiriamali jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kilikuwa na kaulimbiu, “Mustakabali wa MSMEs zinazoongozwa na wanawake: Ushirikishwaji, changamoto na Fursa.” Lengo ni kuwawezesha wanawake wajasiriamali kushiriki kikamilifu katika ajenda ya maendeleo ya muda mrefu chini ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 (Dira 2050).
Akizungumza katika jukwaa hilo, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, amesema MSMEs zinazoongozwa na wanawake ndizo mhimili wa uchumi wa Tanzania, zikichangia kwa kiasi kikubwa ajira, kipato cha kaya na ubunifu wa ndani.
Hata hivyo, bado zinakabiliwa na vikwazo vya kimfumo vinavyozuia ukuaji wao. Ili Tanzania ifikie malengo ya Dira ya 2050, wanawake wajasiriamali lazima wajumuishwe kikamilifu katika mkakati wa ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kikao hicho kilitoa fursa kwa wanawake wajasiriamali kueleza wazi changamoto wanazokumbana nazo, ikiwemo ukosefu wa mitaji nafuu, changamoto za matumizi ya teknolojia za kidijitali, vikwazo vya kisheria na kiutawala, upungufu wa masoko na mifumo dhaifu ya msaada wa biashara.