Kilwa. Majeruhi aliyepata ajali katika basi la Maning Nice iliyotokea jana saa 12 asubuhi, Ahmad Ally, amefariki dunia baada ya kupata ajali katika eneo la Mavuji, wilayani Kilwa, mkoani Lindi, wakati akipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Ally, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40–50, amefariki dunia katika ajali iliyotokea saa 7 usiku kuamkia leo Jumapili, Februari 8, 2026. Ajali ya awali ilitokea Jumamosi, Februari 7, 2026, saa 12 asubuhi na kusababisha vifo vya watu wawili, akiwamo mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Digital leo Jumapili, Februari 8, 2026, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilwa (Kinyonga), Dk Reornad Lucas, amesema kuwa alipokea mwili wa marehemu saa 7 usiku pamoja na majeruhi wawili, ambao walitibiwa na baadaye kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Sokoine).
Dk Lucas amesema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilwa Kinyonga, na majeruhi wamepelekwa katika hospitali ya mkoa wa Lindi.
“Nimepokea mwili wa marehemu saa saba usiku, huku majeruhi wakitibiwa na kupelekwa hospitali ya mkoa kwa ajili ya matibabu zaidi,” amesema Dk Lucas.
Hata hivyo, Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Dk Alexander Makalla, amesema kuwa marehemu alitambulika kwa jina la Ahmad Ally (40–50), na alikuwa akipelekwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Dk Makalla amesema kuwa baada ya kupata ajali walikwenda kuwachukua majeruhi ambao ni muuguzi pamoja na dereva, na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi.
Pia amesema kuwa majeruhi wote wanaendelea vizuri, kwani dereva alipata jeraha la mguu na muuguzi aliumia kwenye paji la uso.
Juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi bado zinaendelea.
Ajali ya kwanza ilihusisha basi la Kampuni ya Maning Nice lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, baada ya kugonga lori lililokuwa limeharibika eneo la Mtange, Manispaa ya Lindi.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Yusuph Salim, alisema hospitali hiyo imepokea miili miwili pamoja na majeruhi 12 saa 1:15 asubuhi.
Alisema kati ya majeruhi hao, wawili walipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi, huku 10 wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
“Tumepokea miili miwili, mmoja ni mwanaume mwenye umri wa miaka 50 na mwingine ni mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
“Miili hiyo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hapa hospitalini, majeruhi 10 wanaendelea na matibabu, na wawili wakipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili,” alisema Salim.