Unguja. Katika juhudi za kuimarisha sekta ya elimu, Serikali imeanisha maeneo saba ya vipaumbele vya utekelezaji wa bajeti ya elimu kwa mwaka 2025/26 ili kutoa elimu bora, huku ikitaja tija iliyoanza kuonekana kufuta rekodi za Zanzibar kushika mkia katika matokeo ya mitihani ya taifa.
Maeneo hayo ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa 1,008, yakiwemo madarasa katika shule za ghorofa 18 na shule za chini, pamoja na kukamilisha madarasa yaliyoanzishwa na nguvu za wananchi.
Pia, ujenzi wa bweni 16 katika mikoa yote ya Unguja na Pemba na kuajiri walimu 18,000.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 8, 2026 kuhusu mageuzi ya elimu Zanzibar, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa, ametaja eneo lingine kuwa ni kuendeleza ujenzi wa kampasi ya kudumu ya Chuo cha Teknolojia cha India Zanzibar (IITM), ikijumuisha ujenzi wa jengo la madarasa na nyumba za walimu.
“Serikali inaendelea kutekeleza azma yake ya kufanya mageuzi makubwa ndani ya sekta ya elimu. Jitihada zinazoendelea ni kuondoa mikondo miwili na kuingia mkondo mmoja,” amesema.
Katika ujenzi unaoendelea, upande wa sekondari umefikia asilimia 81 ya shule kuingia mkondo mmoja kati ya shule 227 za Serikali zilizopo kisiwani hapo, huku shule za msingi asilimia 70 za shule 341 za Serikali zikijiunga na mkondo mmoja.
Kwa upande wa shule za maandalizi, zote zinaingia mkondo mmoja katika shule 263 zilizopo Zanzibar.
Kipaumbele kingine, kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, ni kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuanzisha smart classrooms 25, maabara mbili za STEM (Science, Technology, Engineering, and Mathematics) na maabara mbili kwa ajili ya akili unde (AI).
Pia, zitanunuliwa kompyuta mpakato 4,000 kwa wanafunzi, kompyuta 2,000 kwa maabara, kompyuta 500 kwa walimu wakuu, na smart blackboard 25.
Hatua hizo zinalenga ufundishaji wa kidijitali na mazingira bora ya elimu kwa walimu na wanafunzi, huku jumla ya taasisi 74 za kielimu zimepangwa kuunganishwa na mkonga wa taifa.
Katika mpango huo, Waziri Lela amesema wataajiri walimu 1,800 kukabiliana na uhaba wa walimu katika baadhi ya shule na kupata walimu katika shule mpya zinazoendelea kujengwa.
Katika mageuzi hayo, inaendelea kutekeleza mpango mpya wa umahiri na kidijitali na kuunganisha shule na mkonga wa taifa.
Kuhusu sera na sheria mpya ya elimu, waziri huyo amesema vipo katika hatua mbalimbali, moja ipo katika hatua ya kupitiwa na makatibu wakuu na nyingine ipo Baraza la Wawakilishi. Itakumbukwa kuwa sheria ya elimu inayotumika Zanzibar kwa sasa ni ya mwaka 1982, na mambo mengi yamepitwa na wakati kulingana na mabadiliko ya teknolojia.
Pia, inaanzishwa Tume ya Utumishi ya Walimu, kuanzishwa taasisi ya mafunzo ya amali, na kuimarisha mamlaka ya mafunzo ya amali ili kuthibiti ubora wa elimu ya amali.
“Tunaanzisha mfuko wa elimu, ushiriki wa sekta binafsi katika elimu, na tunaanzisha vyuo katika sekta ili kujenga umahiri zaidi, mathalani kilimo, afya, fedha, taasisi ya Kiswahili Nkrumah, na habari,” amesema. Awali, vyuo hivi vilikuwa chini ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza).
Kutokana na jitihada hizo zinazoendelea, kumeanza kushuhudiwa mabadiliko katika elimu, hususan kwenye ufaulu katika matokeo ya taifa ya kidato cha nne, cha pili na cha saba.
Takwimu za matokeo ya kidato cha nne mwaka 2025 zinaonesha ufaulu umefikia asilimia 91.9 ya watahiniwa 20,764 waliofanya mtihani na kupata madaraja ya kwanza, pili, tatu, na nne, ikilinganishwa na ufaulu wa asilimia 82 mwaka 2024.
“Matokeo haya yanaonesha kuimarika kwa ufaulu mzuri, ambapo idadi ya watahiniwa waliopata madaraja I hadi III imeongezeka kutoka asilimia 30.4 mwaka 2024 hadi asilimia 42.5 mwaka 2025,” amesema Lela.
Kwa mujibu wa waziri huyo, matokeo ya mwaka 2025 yameandika historia ya kipekee sio tu kwa kufikia asilimia 91.9 ya ufaulu, bali pia kwa kushuhudia ufaulu wa daraja la juu.
“Kwa mara ya kwanza Zanzibar tumefanikiwa kuwa na wanafunzi 150 waliofaulu daraja la kwanza kiwango cha alama tarakimu moja (single digit). Kati ya hao, wanafunzi 57 wamefaulu daraja la kwanza wakiwa na alama saba, wanafunzi 42 alama nane, na wanafunzi 51 alama tisa,” amesema Lela.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Khamis Abdulla Said, amesema uwekezaji katika sekta ya elimu unagusa moja kwa moja mustakabali wa Zanzibar.
“Kwani elimu bora hujenga rasilimali watu wenye maarifa, ujuzi, maadili, na ushindani,” amesema Khamis.