Maxime: Mfumo sasa umekubali, yeyote aje tu!

BAADA ya msoto wa muda mrefu bila ushindi, hatimaye juzi Mbeya City ilikata mzizi wa fitina kwa kuikanda TRA United kwa mabao 2-0, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime akitamba kuwa mfumo sasa umekubali na wapo tayari kuvaana na yoyote.

Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, haikuwa na mwanzo mzuri chini ya aliyekuwa kocha Malale Hamsini ambaye alijikuta kifungashiwa virago na nafasi yake kuzibwa na Maxime.

Tangu alipotua kikosini humo, Maxime aliiongoza City mechi tatu akifungwa moja na sare mbili ikiwa ni mwendelezo wa matokeo mabovu ya michezo tisa mfululizo bila kuonja ushindi.

Juzi ikiwa ugenini mjini Tabora, ilionyesha kiwango bora na kufanikiwa kushinda kwa idadi hiyo na kujinasua nafasi za mkiani ikipanda hadi nafasi ya 11 kwa pointi 13 baada ya michezo 14 kwenye Ligi Kuu.

Akizungumzia matokeo hayo, Maxime amesema ilikuwa ni suala la muda kwa vile aliona uwezo wa wachezaji wake namna wanavyocheza kwa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi bila kuzitumia.

Amesema kwa muda mrefu alisubiri waingie rasmi kwenye mfumo akieleza kuwa kwa sasa anaanza kuona mabadiliko na mkakati wao kila mchezo ulio mbele yao ni kupata pointi tatu ili kujiweka pazuri zaidi.

“Si kwamba timu haikuwa inacheza vizuri ni vile matokeo yalikuwa yanagoma, nafasi tulikuwa tunapata ila hatuzitumii hivyo huu ni mwanzo mpya na matarajio yangu ni kuendeleza ushindi,” amesema Maxime na kuongeza;

“Naona sasa mfumo umekubali na niliahidi, tunaenda kujipanga kuhakikisha tunalinda matokeo haya kwa kila mechi inayofuata, bado hatupo sehemu nzuri na tunahitaji kurejesha heshima upya.”

Amesema baada ya mchezo huo wanarejea tena Uwanja wa Sokoine kuwakaribisha Fountain Gate, ambapo watapambana kuondoa gundu kwenye uwanja huo ambao umeonekana kuwa mgumu kwao kupata ushindi.