Dar es Salaam. Huenda Soko la Kariakoo unalolifahamu au kuwahi kulisikia likawa na taswira mpya, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza utaratibu mpya wa maegesho, njia za kusafirisha mizigo na kufunguliwa kwa barabara zinazoingia na kutoka sokoni humo.
Lingine aliloelekeza ni kujengwa kwa maeneo ya watoto kucheza, kuimarishwa ulinzi, viwango vya ubora wa bidhaa na kuhakikisha mfanyabiashara anayetaka kusafirisha mzigo mkubwa, asilazimike kuisaka huduma hiyo nje ya soko hilo.
Kauli hiyo ya Samia inakuja, katika kipindi ambacho Soko la Kariakoo limekabiliwa na msongamano wa wafanyabiashara na mpangilio mbaya wa shughuli, unaosababisha baadhi ya barabara zisipitike.
Hata hivyo, mabadiliko ya soko hilo yamekuja baada ya Serikali kulijenga upya kwa Sh28 bilioni, kutokana na kuungua moto Juni mwaka 2021 na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara na Serikali.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam leo, Jumapili Februari 8, 2026 alipohutubia katika hafla ya ufunguzi wa Soko la Kariakoo.
Mkuu huyo wa nchi ametaka kuwe na mpangilio mzuri wa maegesho, njia za kusafirisha, kupakia na kupakua mizigo kwa kuwa kutakuwa na magari yanayopeleka mizigo sokoni humo.
“Maguta nayo yapangiwe utaratibu maalumu wa kuingia na kutoka sokoni. Kwa watoto wangu bodaboda ambao wataleta wateja au kuwatoa na wenyewe wapangiwe vizuri,” amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Soko Kuu jipya la Kariakoo, Ilala Jijini Dar es Salaam tarehe Februari 8, 2026.
Amesema hakuna yeyote atakayekosa fursa ndani ya soko hilo, hivyo ni muhimu kuwe na mpangilio mzuri kwa kila mmoja, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa usalama kwa wafanyabiashara na wateja.
Mkuu huyo wa nchi, ameagiza sokoni humo, kuimarishwe viwango vya bidhaa zitakazouzwa ili viwe stahiki kwa kuwa kuna wateja wanaotoka ndani na nje ya nchi.
“Watu wa TBS (Shirika la Viwango la Taifa) na watu wa TMDA (Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba) tuhakikishe bidhaa zinazowekwa hapa zina viwango ili soko letu hili liaminike kitaifa na kimataifa,” amesema.
Ametaka kuwepo huduma za kimataifa kwa kuwa Kariakoo ni soko la kikanda, hivyo mteja akifika apate huduma za kifedha, kulipia kodi na usafirishaji katika eneo moja.
“Tunaposema usafirishaji tunamaanisha magari ya ndani na maguta, lakini usafirishaji wa bidhaa kwenda nje. Watakuja watu wananunua mizigo mikubwa kwenda nje, wakute usafiri upo ndani hapa,” amesema.
Ametaka mawakala wa kutoa huduma za usafirishaji nje ya nchi, wawepo ndani ya soko hilo ili wafanyabiashara wamalize mambo yao ndani, huku akiitaka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kusimamia yote.
Jambo lingine, amesema mbali na eneo la kunyonyeshea lililojengwa, kujengwe vyumba vya malezi ya watoto, kwa kuishirikisha sekta binafsi, ili mama zao wanaofanya biashara wapate muda wa kufanya shughuli zao.
“Ninyi (uongozi wa soko) mtatoa eneo, lakini akitokea mtu binafsi kuweka kitengo hicho cha kulea watoto ambacho kitaangaliwa vizuri, vifaa vyote, watoto watakula vizuri, sekta binafsi karibuni,” amesema.
Ametaka Kariakoo liwe soko la mfano wa masoko mengine nchini kwa ufanisi wa biashara na uimara wa mifumo, huku akisisitiza usimamizi wa uthabiti na uendelevu wa mifumo ya kisasa, ikiwemo ya zimamoto na wafanyabiashara wafunzwe jinsi ya kutumia mitungi ya kuzimia moto.
‘Tusipangane kwa kujuana’
Ameitaka Tamisemi ihakikishe utaratibu wa kuwarudisha wafanyabiashara waliokuwepo awali katika soko hilo unafanyika bila kujuana, upendeleo wala ukiritimba.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa kuashiria uzinduzi wa Soko Kuu jipya la Kariakoo, Ilala Jijini Dar es Salaam Februari, 8, 2026.
“Nakumbuka nilikuja kutembelea soko hili, nilikuta wafanyabiashara wengi wamebanana na wengine nje ya soko vibandavibanda vingi. Ile ilikuwa inaonyesha uhitaji wa kuwa na soko la aina hii,” amesema.
Amesema mbali na soko lililoungua, limejengwa lingine la ghorofa sita na waliokuwa nje, wawekwe kwenye nafasi zitakazobaki bila upendeleo.
Viongozi wasihodhi maeneo
Samia amewataka viongozi wa Jiji la Dar es Salaam, wasihodhi vizimba katika Soko la Kariakoo na kuwakodishia wafanyabiashara, badala yake shughuli hiyo ifanywe na Shirika la Masoko la Kariakoo.
“Hapa nazungumza na wakubwa wa Jiji la Dar es Salaam, nisingependa kusikia ninyi wenyewe ndio mnahodhi maeneo mnakodisha watu. Shirika lenyewe la Masoko Kariakoo ndilo liwe linakodisha watu humu na ukodishaji uwe wa wazi na mapato yawe ya wazi,” amesema.
Amesema kumekuwa na malalamiko ya mifumo ya tozo na ada za pango la maeneo ya biashara, akiwataka wataalamu wa Tamisemi kukaa na wafanyabiashara na kuja na mapendekezo yatakayolinda pande zote.
Amesema wafanyabiashara lazima walipe pango lakini lisiwe la kuwaumiza na lisiwe chini, kwa kuwa hilo ni soko la hadhi ya kimataifa.
“Asiyeweza kulipa asubiri tumalize maeneo mengine. Niliambiwa wanangu machinga, walitaka kuingia na fulana zao waniambie mama tunasubiri soko la kule Jangwani. Lakini mmewazuia kuingia, nataka kuwaambia wanangu sauti zenu nimezisikia na tupo katika hatua za kulijenga,” amesema.
Ameutaka uongozi wa soko kuwa na orodha ya wafanyabishara wote watakaokuwepo ndani ya soko na ulipaji kodi ufanywe kwa mifumo ili asiwepo hata mmoja ambaye hatalipa.
Ametaka uwazi kwenye mapato na matumizi na ndio sababu awali soko hilo lilichomwa moto.
“Yanapokua hayapo wazi, unapokuja ukaguzi, jambo la maana kwa haraka watu kuhifadhi nafasi yao ni kutia moto ili taarifa na rekodi zisiwepo,” amesema.
Jambo lingine, amesema mazingira yanayozunguka soko na muingiliano wa shughuli za biashara umeleta msongamano kwa watu akitaka kujifunza kutoka kwa masoko ya wengine nje.
Ametaka mpangilio wa mizigo wakati wa kuingia na kutoka ili kupunguza msongamano, huku akidokeza kwa kuwa kuna maji sokoni humo kwa sasa, usafi uimarishwe maeneo yote.
Lingine aliloelekeza ni kuimarishwa kwa huduma ya mawasiliano kwa mtu anapokuwa ndani ya soko, kwani kwa sasa amesikia kuna shida ya mtandao kupatikana.
Katika ufunguzi wa soko hilo, Samia amesema anatambua juhudi za machinga na mawinga katika kujitafutia kipato ndio maana kipaumbele cha Serikali ni kurasimisha biashara zao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, katika eneo la jiwe la ufunguzi wa Soko Kuu jipya la Kariakoo, Ilala Jijini Dar es Salaam Februari, 8, 2026.
“Huko nyuma tulikuwa tunajua wamachinga, kumbe kuna neno jipya limejitokeza la mawinga na nilikua nazungumza na waziri hapa mawinga ni kina nani. Akanambia ni wale wanaofanya survey Kariakoo bidhaa fulani hazipo ndani ya soko wanakwenda kuzichukua ziliko na wanawaletea wafanyabiashara ndani ya soko.
“Au wanaangalia huko nje bidhaa gani hazipo lakini zipo Kariakoo kwa wingi wanachukua na kupeleka kwenye maeneo mengine,” amesema.
Amezitaka halmashauri kuweka miundombinu rafiki ya kufanya biashara kwa vijana popote Dar es Salaam na kwingineko
“Waziri Mkuu ameagiza ile asilimia 10 inayotoka kwa vijana, wanawake, iongezwe iwe 15 ili ile tano iende ikawajengee miundombinu ya kufanyia biashara vijana wetu,” amesema.
Amesema soko la kariakoo haliwezi kuendeshwa kwa mifumo ya zamani, linahitaji mageuzi ya kiutawala, mtazamo na usimamizi unaozingatia huduma bora, nidhamu na ufanisi na kwamba Tamisemi isimamie hilo.
Amesisitiza miundombinu imejengwa kwa gharama kubwa zilizotokana na kodi za wananchi ni wajibu wa wananchi kulilinda na kulitumia kwa tija soko ili liendelee kuwahudumia wafanyabiashara wote ndani na nje.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Rais Samia amemwelekeza kuhakikisha kila Jiji, Manispaa na Halmashauri yenye wafanyabiashara wengi itengwe asilimia tano kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya masoko.
Ameeleza asilimia tano hizo, ziongezwe kutoka zile 10 za mapato ghafi ya halmashauri zinazotolewa kuwakopesha wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na wenye ulemavu asilimia mbili.
Katika kulitekeleza hilo, amesema ameshakaa na wizara zinazohusika ikiwemo ya fedha, kuhakikisha wafanyabiashara wanapata maeneo ya kufanyia shughuli zao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kuanza huduma katika Soko la Kariakoo kutaambatana na kufunguliwa na barabara zote zinazoingia na kutoka sokoni humo.
Hatua hiyo kwa mujibu wa Chalamila, inalenga kuongeza usalama wa soko hilo, urahisi wa huduma na kurahisisha uokozi inapotokea changamoto.
Amesema tayari ameshazungumza na wafanyabiashara wote kuanzia sasa barabara zote ndani ya soko hilo zitafunguliwa, ingawa anafahamu maelekezo hayo yanaweza kuwa machungu kwa baadhi ya watu.
“Inawezekana lisiwe jambo zuri na yanaweza kuwa maelekezo machungu kwa wafanyabiashara, lakini huwezi kujenga nyumba yenye thamani ukaziba barabara. Naamini diplomasia itaendelea kutumika pasipo kutumia nguvu kwamba barabara zitabaki wazi,” amesema.