Oura atoa kauli nzito Simba

LICHA ya kucheza mechi tano bila kuibuka na ushindi wowote katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, winga mpya wa Simba, Anicet Oura, amewatuliza mashabiki wa klabu hiyo akiwaambia anaamini nyakati nzuri zinakuja mbele yao kutokana na kazi kubwa inayofanywa na wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo.

Oura ambaye aliisawazishia Simba katika mechi iliyopita huko Angola dhidi ya Petro Atletico, amesema kuwa pointi hiyo moja ni ushahidi wa juhudi za kikosi chote, hasa baada ya kucheza wakiwa pungufu ya mchezaji mmoja, Shomary Kapombe aliyepata kadi mbili za njano.

“Matokeo haya si mwisho wa kila kitu, tunaendelea kufanya kazi kwa pamoja na najua nyakati nzuri zinakuja,” amesema Oura.

Winga huyo aliongeza kuwa timu ipo kwenye mwelekeo mzuri.  “Wakati mwingine unaweza kurudi nyuma hatua mbili lakini pia unaweza kupiga hatua tano mbele. Hii ndiyo hali ya soka,” amesema.

Hata hivyo, matokeo ya awali yameifanya Simba kuburuza mkia katika msimamo wa kundi D, ikiwa na pointi mbili tu.

Kundi hilo linaongozwa na Stade Malien yenye pointi nane huku Esperance Tunis na Petro Atletico wakifuata katika nafasi ya pili na tatu, kila mmoja akiwa na pointi sita.

Simba itakamilisha ratiba yake katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza nyumbani dhidi ya Stade Malien, mechi ambayo watatakiwa kumaliza kwa heshima hatua hiyo.

Mechi dhidi ya Petro Atletico ilikuwa ya tatu mfululizo kwa Oura kuichezea Simba tangu ajiunge nayo katika dirisha la usajili ya Januari akitokea Ulaya ambako alikuwa akiichezea IF Gnistan ya Finland.

Alianza kukipiga dhidi a Mashujaa katika ligi ambapo Simba ilishinda kwa mabao 2-0 kisha Esperance Tunis (2-2) na Petro Atletico (1-1) ambazo zote Mnyama ametoka sare.

Ametumika kwa jumla ya dakika 213.