Mabula akiri ngoma mzito Azerbaijan

KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Shamakhi FK ya Ligi Kuu Azerbaijan, Alphonce Mabula amesema mzunguko wa pili wa ligi hiyo umeanza kwa kasi kubwa, huku ushindani ukiwa mkali zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Huu ni msimu wa pili wa kiungo huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars kuitumikia timu hiyo. Msimu uliopita alicheza nusu msimu alipojiunga na Shamakhi akitokea FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu ya Serbia alikocheza kwa misimu miwili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mabula amesema baada ya mapumziko ya nusu msimu timu nyingi zimerudi zikiwa zimefanyia kazi mapungufu yao, hali iliyofanya kila mechi kuwa ngumu.

“Mzunguko wa pili umeanza kwa kasi sana. Kila timu imejipanga vizuri, hakuna mechi rahisi kila mechi unahitaji pointi ili uweze kujiweka kwenye nafasi nzuri,” amesema Mabula na kuongeza:

“Kila kosa dogo unaadhibiwa ligi imekuwa na kasi, presha ni kubwa na unahitaji umakini wa hali ya juu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mechi maana huku hakuna ugenini wala nyumbani.”

Mabula aliongeza anaendelea kupambania nafasi ya kudumu kikosini na kuisaidia Shamakhi kufikia malengo ya kumaliza ndani ya nafasi nne za juu msimu huu.

“Kucheza hapa kunakupa uzoefu mkubwa ni ligi inayokulazimisha kufikiria haraka, kucheza kwa nidhamu na kupambana kila dakika. Naamini nikiendelea kukiwasha basi nitapata pia nafasi ya kuonekana na kujumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa.”

Shamakhi iko nafasi ya nane katika msimamo wa ligi. Kwenye mechi 18 imeshinda sita, sare tano na kupoteza mechi saba ikikusanya pointi 23.

Kati ya mechi sita ilizocheza imechukua pointi sita kwa Sabah Baku ambayo inaongoza ligi na pointi nne kwa Qarabag iliyopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.