Watatu wauawa katika majibizano ya risasi na Polisi Simiyu

Bariadi, Simiyu. Watu watatu wanaodaiwa kuwa majambazi wamefariki dunia baada ya majibizano ya risasi na Kikosi Maalumu cha Kuzuia na Kupambana na Uhalifu cha Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, kwa madai walikuwa wakijaribu kuvunja na kuiba fedha katika jengo la Simiyu Money Service mjini Bariadi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe amesema tukio hilo limetokea saa 8:30 usiku wa kuamkia leo Februari 8,2026  katika mtaa wa NMB, Kata ya Malambo. Amesema Polisi walipokea taarifa kuwa majambazi hao walikuwa wakivunja milango ya jengo linalotumika kutoa huduma za miamala ya fedha kwa kampuni za simu na taasisi za kifedha.

“Baada ya kupokea taarifa, kikosi maalumu kilifika eneo la tukio. Wakati watuhumiwa walipobaini wanafuatiliwa na polisi, walianza kufyatua risasi, hali iliyolazimu askari kujibu mashambulizi hayo,” amesema Kamanda Swebe.

Ameongeza kuwa majibizano hayo yalisababisha watuhumiwa wote watatu kujeruhiwa na kufariki dunia walipokuwa wakiwahishwa hospitali kwa matibabu.

Katika upekuzi, polisi walikamata silaha moja ya AK-47 ikiwa na risasi nane ndani ya magazini. Aidha, watuhumiwa walikamatwa wakiwa na shilingi 300 za Kenya, noti moja ya shilingi 5 ya Misri, pamoja na tiketi za usafiri kutoka Migori kwenda Silari na kutoka Silari kwenda Lamadi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limesema linaendelea na operesheni na misako mbalimbali mkoani humo kwa lengo la kudhibiti na kukomesha vitendo vya uhalifu. Pia limewashukuru wananchi kwa ushirikiano wao katika kutoa taarifa zinazosaidia kubaini na kuzuia uhalifu, huku likiwataka watu wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja, likisisitiza kuwa hasara ya uhalifu ni kubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.