Ulega: Uchunguzi mkataba mkandarasi wa barabara Kagera umeanza

Arusha. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema mchakato wa kuvunja mkataba na mkandarasi wa kampuni kutoka China anayejenga barabara ya Omurushaka- Kyerwa mkoani Kagera yenye urefu wa kilomita 50 umeanza.

Kauli hiyo imekuja zikiwa zimepita siku tisa baada ya Waziri Ulega kufanya ziara mkoani humo Januari 31,2026 na kuagiza kuvunjwa mkataba wa kampuni hiyo baada ya kuonekana ujenzi wake unasuasua.

“Natoa maelekezo kwa Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) kutoka wizarani mpitie taratibu za kuvunja mkataba kwa mkandarasi huyo ndani ya mwezi mmoja ili tumchukulie hatua za kisheria,” alisema Ulega.

Jana Jumapili Februari 8,2025 akiwa mkoani Arusha kutoa tathimini ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu utendaji kazi wa wizara hiyo na kujibu maswali ya wanahabari, Ulega amesema watalaamu wa Tanroads wapo kazini kukagua suala la mkandarasi huyo.

“Wanakagua hatua kwa hatua ikiwa ni pamoja na fedha alizolipwa zaidi ya Sh9 bilioni nazo zitakaguliwa tujue amezitumiaje. Haya ndio maelekezo ya Rais Samia ya kuhakikisha kila shilingi ya Mtanzania inayotumika katika mradi ikaguliwe,” amesema.

“Hivi sasa watalaamu wetu wanakagua ile Sh9 bilioni imetumikaje maana ukienda eneo la mradi hakuna lami hata ya kilomita moja kwa miezi yote tangu Januari 2024,” amesema Ulega.

Amefafanua kuwa maelekezo yake kwa Mkoa wa Kagera ikibainika mkandarasi huyo ametumia fedha vibaya atafunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi, na haitaishia kwake bali wote watakaohusika kwenye jambo hilo.

Msingi wa Waziri Ulega kueleza hayo, umetokana na swali aliloulizwa nani alaumiwe kati ya mkandarasi na msimamizi kuhusu miradi kutokamilika kwa wakati.

Waziri Ulega ametoa tathimini hiyo katika mkutano wake wa hadhara ulioanza jioni na kumalizika usiku eneo la King’ori wilayani Arumeru ukienda sambamba na uzinduzi wa uwekaji wa taa za barabarani katika kata hiyo.

Waziri huyo amejenga hoja akieleza namna Serikali na wizara hiyo zilivyodhamiria kushughulikia nidhamu na ubadhirifu wa fedha za umma, akieleza kuwa jitihada hizo zimeshaanza kuonekana kwenye miradi mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amesema Serikali imefanya juhudi  za kuwapa zabuni za miradi mbalimbali makandarasi wazawa ili kuhakikisha mzunguko wa fedha unakuwa mzuri kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa Waziri Ulega, miradi ya dharura 81 yenye thamani ya zaidi Sh500 bilioni kati ya hiyo 60 imetekelezwa na makandarasi wazawa iliyobaki wa kigeni.

Miongoni mwa miradi hiyo ya dharura ni pamoja na ujenzi wa madaraja, barabara, uwekaji wa taa za barabarani, uinuaji wa matuta.

Mbali na hilo, Ulega amesema wataalamu wake wanachakata utaratibu utakaowawezesha makandarasi wa ndani kushiriki miradi mikubwa ya kuanzia Sh200 bilioni inayofadhiliwa na wahisani kutoka nje.

Kwa mujibu wa Ulega, hivi sasa kazi yoyote isiyozidi Sh50 hairuhusiwi kupewa mkandarasi mgeni, badala yake itafanywa na wazawa, akisema hayo ni maelekezo ya Rais Samia yanayotekelezwa kwa vitendo na wizara hiyo.

Katika mkutano huo, Waziri Ulega amesema katika kipindi cha kuanzia Novemba hadi Januari 2025 wizara hiyo imepokea Sh511 bilioni kati ya hizo Sh125 zilitoka katika Mfuko wa Barabara na kwenda kuwalipa makandarasi wadogo.

Baada ya mkutano wake na wanahabari, Ulega alizindua mradi wa taa 150 zilizowekwa eneo la King’ori hatua itakayowezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa uhakika na ufanisi.

Mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), Joshua Nassari amesema ndani ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan kuna miradi mbalimbali imetekelezwa na kuleta ahueni kwa wananchi wa jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa madaraja.

Nassari amesema kulikuwa na changamoto ya makalavati na madaraja, lakini ndani ya siku 100 Wizara ya Ujenzi imetatua changamoto hiyo, hivyo wanaishukuru Serikali kwa jitihada hizo.

“Taa hizi zitasaidia kuimarisha ulinzi na  usalama wa watu wetu tunakushukuru sana Waziri ( Ulega), tumeokoa vifo vya watu waliokuwa wakisombwa na maji kwa kukosekana madaraja,” ameeleza Nassari.

Waziri Ulega amesema kwa sasa Serikali inafikia au ipo kwenye mpango unaopikwa wa kujenga barabara za kulipia ‘express way’ kuelekea viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere  (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro( KIA).