Hizi ndio shughuli zitakazofanyika mkutano wa pili Baraza la Wawakilishi

Unguja. Wakati mkutano wa pili wa Baraza la 11 la Wawakilishi ukitarajia kuanza Jumatano Februari 11, 2026 mambo 13 yanatarajiwa kufanyika ndani ya mkutano huo huku ukitajwa kuwa na nguvu zaidi kutokana na ongezeko la wapinzani barazani.

Katika mkutano huo, ambao utakuwa na wajumbe 178 unatarajiwa kuwa na mvuto zaidi ikilinganishwa na mkutano uliopita baada ya kuwamo wawakilishi wa upinzani 14 wanaotokana na Chama cha ACT Wazalendo ikilinganishwa na wawakilishi wanne waliokuwamo katika baraza la 10.

Katika mkutano huo, yanatarajiwa kuulizwa maswali ya msingi 220 kutoka kwa wawakilishi.

Ongezeko la wapinzani hao unatajwa kuibua hoja kinzani kutoka upande wa pili katika mkutano huo. Licha ya Chama cha ACT Wazalendo bado kutoigia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini wawakilishi wa chama hicho waliochaguliwa majimboni wataendelea na shughuli zao kama kawaida barazani.

Mnajimu wa upinzani Barazani, Profesa Omar Fakih ambaye ni mwakilishi wa Pandani amesema wamechaguliwa na wananchi kwa hiyo wataendelea kuhudhuria vikao kama kawaida, wakati chama kikiendelea na utaratibu wa kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Amesema kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanaibana Serikali katika mambo wanayoona  hayaendi sawa.

Mchambuzi wa siasa Zanzibar, Ali Makame amesema baraza la wakati huu linaweza kuwa la kipekee kutokana na wingi wa upinzani, kwani wanaweza kuwa na sauti na wakasikika tofauti na linapokuwa la upande mmoja.

“Tunachotarajia kuona katika baraza hili ni hoja za kimageuzi, zinazolenga masilahi ya Wazanzibari na nchi yenyewe badala ya watu kuzungumzia mambo yao binafsi,” amesema.

“Zaidi tunataka kuona mawazo kinzani, kuongezeka kwa upinzani nadhani inaweza kutumika kama kete kwa masilahi ya wananchi, na pale zinapokuwapo hoja nzuri ni vyema zikachukuliwa na kuzingatiwa kwa masilahi ya Zanzibar,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo utakaofanyika kwa takribani wiki mbili utajadili hotuba ya uzinduzi wa baraza la wawakilishi la 11 aliyoitoa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi Novemba 10, 2025.

Shughuli nyingine itakayofanyika katika mkutano huo ni kujadili na kupitisha mwelekeo wa mpango wa Taifa mwaka 2026/27.

Kwa mujibu wa Katibu wa Baraza la Wawakilsihi, Raya Issa Msellem katika mkutano huo pia kutakuwa na chaguzi mbalimbali zikiwamo za kuchagua wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Pia utahusisha uchaguzi wa wabunge watano la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Baraza la wa Wawakilishi.

“Mkutano huu utahusisha uchaguzi wa viongozi wa chama cha wabunge wa nchi za Jumuiya ya Madola Kanda ya Zanzibar (CPA), uchaguzi wa chama cha wabunge wanawake wa nchi za Jumuiya ya madola Kanda ya Zanzibar (CWP),” amesema.

Kingine utafanyika uchaguzi wa viongozi wa Umoja wa Wanawake wa Baraza la Wawakilsihi Zanzibar (Uwawaza), uchaguzi wa viongozi wa mtandao wa wabunge wa Afrika wa kupambana na Rushwa (APNAC) Kanda ya Zanzibar.

Shughuli nyingine kwa mujibu wa Baraza hilo, ni uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya ya wawakilishi kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi Zanzibar, na uchaguzi wa viongozi jumuiya ya wawakilishi kuhusiana idadi ya watu na maendeleo Zanzibar.