MAKAMU WA RAIS AZINDUA MPANGO WA USHIRIKIANO KATI YA TAASISI ZA ELIMU NA VIWANDA

………..

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt.
Emmanuel Nchimbi ametoa
wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Vyuo, kuwekeza
katika tafiti hususan za sayansi na teknolojia ili kuinua viwango vya tafiti na
ubora wa elimu nchini.

 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa ushirikiano
kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri, uliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

 Amesema Kupitia Mpango huo, sekta binafsi
inaweza kuchangia maendeleo ya elimu kwa kufadhili tafiti na kutoa ufadhili kwa
wanafunzi wa fani mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko la ajira.

 

Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Taasisi za elimu na Sekta binafsi nchini kuzingatia maendeleo ya
kasi ya sayansi na teknolojia duniani katika utekelezaji wa Mpango huo. 

Amesema Vyuo na Sekta
binafsi vishirikiane kubaini
ujuzi
muhimu unaohitajika sasa na siku zijazo hususan katika fani za sayansi,
teknolojia, ubunifu, tiba, uhandisi na hesabu ili kuwezesha vijana kushindana
na kupata nafasi katika soko la ajira 
nchini na kimataifa.

 

Makamu wa Rais amesema ushirikiano baina ya
Taasisi za elimu na Viwanda ni hitaji la lazima katika dunia ya leo, kwa
kuwa  Vyuo haviwezi tena kuwa visiwa vya
nadharia, na viwanda haviwezi kukua bila nguvukazi yenye ujuzi unaoendana na
teknolojia na ushindani wa soko.

Ameongeza kwamba, Serikali
ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele cha kimkakati katika kukuza ujuzi, stadi,
maarifa na sifa za kuajirika au kujiajiri miongoni mwa vijana na wahitimu wa
ngazi mbalimbali za elimu, ikitambua kwamba maendeleo endelevu ya Taifa
hayawezekani bila kuwa na rasilimaliwatu iliyoelimika na yenye uwezo wa
kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

Amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa ya sera na mitaala ya elimu
katika ngazi zote kwa lengo la kuujenga mfumo wa elimu ulio mnyumbufu, jumuishi
na unaoendana na vipaji, mwelekeo na mahitaji halisi ya soko la ajira, huku
ikizingatia mabadiliko ya teknolojia na ushindani wa kitaifa na kimataifa.

Uzinduzi wa Mpango huo ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,
ambapo aliahidi kuanzisha Mpango wa pamoja kati ya Waajiri, Vyuo vya ufundi
stadi na Vyuo Vikuu kwa lengo la kulinganisha mafunzo na mahitaji halisi ya
sekta za kipaumbele za Taifa,
ndani ya siku 100 baada
ya kuapishwa kwake.

Pamoja na mambo mengine, Mpango wa ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na
Viwanda unalenga kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya utoaji wa elimu na
utendaji kazi, kwa lengo la kulinganisha mafunzo na mahitaji ya sekta za
kipaumbele kama nishati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na
viwanda vya kuongeza thamani. Aidha, Mpango unaweka msingi thabiti wa kujenga
kizazi cha wahitimu wenye uwezo wa kuajirika, kujiajiri na kushiriki kikamilifu
katika maendeleo ya Taifa kwani umedhamiria kubadilisha mfumo wa elimu ya
nadharia kwenda mfumo unaozingatia ujuzi, vitendo, ubunifu na uzalishaji mali.

Uzinduzi huo, umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge, Dini
pamoja na wadau wa maendeleo. Wengine waliohudhuria ni pamoja na Waajiri na
Wamiliki wa Viwanda, Wakuu wa Taasisi mbalimbali, Wakuu wa Vyuo pamoja na
Wanafunzi.