Lissu aibua mapya mahakamani ya viongozi Chadema

Dar es Salaam. Akiwa ametimiza zaidi ya siku 300 rumande, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameibuka na malalamiko mapya akidai uongozi wa Gereza la Ukonga umempiga marufuku kutembelewa na viongozi na wanachama wa chama chake.

Pia, amelalamikia kunyimwa faragha katika mawasiliano na mawakili wake, jambo alilowahi kulilalamikia awali, akidai kuwa tatizo hilo limerudi tena.

Katika hatua nyingine, Lissu amelalamikia namna kesi yake ya uhaini inavyoendeshwa, akidai kuwa inacheleweshwa huku ikiwapoza majaji na mawakili wa Serikali wanaoiendesha kesi hiyo kwa kuwatoa lawama hizo.

Jamhuri imejibu hoja za pingamizi la Lissu kuhusu uhalali wa mashahidi wa Jamhuri kutoa ushahidi bila kuonekana, ambapo mahakama imepanga kutoa uamuzi kesho Jumatano, Februari 11, 2026.

Lissu ametoa malalamiko hayo leo, Jumatatu Februari 9, 2026, kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa kesi yake katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam. Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kutokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali.

Kesi hiyo, inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka. Hata hivyo, kabla ya Jamhuri kuanza kujibu hoja za pingamizi lake kuhusu uhalali wa mashahidi kutumia kizimba maalumu, Lissu akaibua madai na malalamiko yake ikiwa ni pamoja na kucheleweshwa kwa kesi yake.

Kuzuiwa kutembelewa na wanachama

Lissu amedai kuwa kwa sasa uongozi wa Gereza la Ukonga, anakohifadhiwa, umepiga marufuku kutembelewa na viongozi na wanachama wa Chadema tofauti na ilivyokuwa awali. Amedai kuwa awali alikuwa anatembelewa na ndugu, marafiki na viongozi na wanachama wa Chadema, lakini baada ya Novemba 12, 2025, aliitwa kwa Mkuu wa Gereza akaambiwa kuwa ni marufuku kutembelewa na viongozi na wanachama wa Chadema.

“Sasa nchi hii ni ya vyama vingi na mimi ni kiongozi wa Chadema kama chama halali, lakini wamepigwa marufuku,” amesema Lissu na kuongeza kuwa magereza ni taasisi ya umma hivyo haina mamlaka kubagua nani anaruhusiwa kuingia gerezani na nani haruhusiwi.

Vilevile, amesisitiza malalamiko yake ya kutokuwa na faragha katika mawasiliano na mawakili wake wanapomtembelea. Amedai kuwa malalamiko hayo si mapya kwani alishawahi kuyatoa mahakamani hapo na kwamba kwa sasa tatizo hilo limerudi. Ingawa kanuni za magereza zinatoa haki kwa wafungwa na mahabusu kufanya mawasiliano bila kuingiliwa, Lissu amesema kwa sasa mazungumzo yake na mawakili wake yamekuwa yakisimamiwa na maofisa magereza.

“Kwa hiyo waheshimiwa majaji nawapa taarifa mtaona ni hatua gani za kuchukua kuhakikisha sheria inatekelezwa na sisi wafungwa na magereza,” amesema.

Lissu amedai kuwa kesi yake inacheleweshwa kwa kiasi kikubwa, lakini hakulaumu majaji wala mawakili wa Serikali wanaoiendesha kesi hiyo. “Leo ni siku ya 307 tangu niwekwe mahabusu, miezi 10 wiki 44 niko mahabusu. Katika siku zote hizi kesi imesikilizwa kwa siku 14 tu na leo ni siku ya 15. Kuna siku 88 ambazo kesi haijasikilizwa kabisa, niko gerezani hakuna kinachoendelea,” amesema.

Amesema tatizo linalochelewesha kesi ni utaratibu wa kuendesha kesi kwa vikao maalumu (sessions) vinavyopangwa na Jaji Mkuu. “Na hilo si tatizo lenu wala la mawakili wa Serikali bali la hao wanaoamua kwamba kesi ziendeshwe kwa sessions,” amesema Lissu.

Amesema kuwa uhaini ni kosa la kipekee, si kama kughushi maandishi au wizi wa kuku kama Ibara ya 28(4) ya Katiba ya Tanzania inavyolitaja, hivyo haliwezi kuendeshwa sawa na mashauri mengine. Amesema kesi yake ni ya tatu ya uhaini nchini, ikitanguliwa na Grey Likungu na wenzake tisa wakiwemo mawaziri na wanajeshi, na ya pili ya Hatib Gandhi.

Kesi za Likungu na Gandhi zilisikilizwa kwa muda mrefu, likiwa na mashahidi wengi, lakini kesi ya Lissu, licha ya kuwa na mashahidi watatu kati ya 30, bado inasikilizwa kwa majaji watatu, jambo linalochelewesha utaratibu.

Majibu ya Jamhuri pingamizi la Lissu

Kuhusu hoja za Lissu juu ya uhalali wa mashahidi wa Jamhuri kutoa ushahidi bila kuonekana, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ameiomba mahakama kutupilia mbali hoja zake akidai kuwa hazina mashiko. Lissu alipinga shahidi wa nne na wengine waliokuwa wamelindwa, akidai kizimba kilichotumika hakikutajwa katika kanuni za Ulinzi wa Mashahidi.

Katuga ameeleza kuwa mashahidi waliolindwa wanaweza kutumia vifaa vya kiteknolojia, ikiwa ni pamoja na kizimba maalumu, na hoja za Lissu hazina msingi wa kisheria. Amesema kanuni za ulinzi zinaweza kutumika hata kwa kurudi nyuma, na sheria husika ilitangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali Namba 7 la Septemba 25, 2018.

Baada ya kusikiliza hoja zote, mahakama imeahirisha kesi hiyo na kupanga kutoa uamuzi wa pingamizi la Lissu Jumatano, Februari 11, 2026.