Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia huduma zinazotolewa na madalali na mawinga, wakidai kwamba wamekuwa chanzo cha kupanda kwa bei za bidhaa au huduma sokoni, jambo linalowaumiza walaji wa mwisho.
Wanasema mawinga wa masokoni na madalali wa vyumba, fremu za biashara na nyumba hupandisha bei za huduma na kufanya baadhi ya watu kushindwa kumudu gharama hizo hasa kwa huduma muhimu.
Jana, Februari 8, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akizindua Soko la Kimataifa la Kariakoo, alizungumzia kundi la vijana wanaoitwa mawinga, akionesha nia ya kulitambua kundi hilo na kuelekeza kuwekwa utaratibu mzuri wa kufanya kazi zao.
Rais Samia alieleza utambuzi wa kundi hilo ambalo awali halikujulikana rasmi kwakumezwa na neno maarufu wamachinga, lakini sasa limejitokeza rasmi kwa neno jipya mawinga.
“Mawinga ni vijana wanaofanya survey (utafiti) ndani ya Kariakoo, wakibaini bidhaa ambazo hazipo sokoni na kisha kuzitafuta nje ya soko ili kuwaletea wateja,” alifafanua Rais Samia, akisisitiza kuwa Serikali inatambua juhudi za vijana hawa kujitafutia kipato, na ndiyo maana imeweka kipaumbele katika kurasimisha biashara zao ili ziwe endelevu na zenye tija.
Katika hatua inayoashiria uhitaji wa kurasimishwa na kuwekewa taratibu za kisheria kwa kundi hilo katika ufanyaji kazi wake, baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wanasema limekuwa kikwazo mtaani kwani wapo wanaoshindwa kupata vyumba vya kupanga, fremu za biashara, viwanja na bidhaa sokoni kutokana na kutakiwa kulipa fedha zisizo rasmi na madalali na mawinga hawa.
Shinikizo hilo la gharama lisilo rasmi, limekuwa kikwazo kwa wananchi wa kawaida, na ongezeko la bei linalozuia baadhi yao kupata mali muhimu kwa wakati unaofaa.
Anna Mushi, mkazi wa Temeke, Dar es Salaam, amesema alishindwa kupata fremu ya biashara katika stendi mpya ya Buza (Kwa Mama Kibonge), inayolipiwa Sh50,000 kwa manispaa, akisema kuipata alitakiwa kulipa Sh5 milioni kwa dalali ili kumuunganisha kupata huduma hiyo.
“Wengi tumeshindwa kupata fremu za stendi mpya ya Buza. Tatizo siyo gharama za fremu, lakini kuzipata kuna watu katikati wanaomba hadi Sh10 milioni kumpangisha mtu,” amesema.
Amesema hiyo inawanyima wananchi na wafanyabiashara wadogo fursa ya kufanya biashara zao hasa katika maeneo rasmi yaliyoandaliwa kwa gharama kubwa na Serikali na hivyo kukosa kipato chao na mapato ya Taifa kwa ujumla.
Neema Kweka, alipozungumza na Mwananchi akiwa sokoni Kariakoo jijini Dar es Salaam leo Februari 9, 2026, amesema bidhaa zinakuwa na bei ghali kutokana na mawinga wanaoshirikiana na wafanyabiashara.
Amesema mawinga hao wanawasiliana na wafanyabiashara kisha wanawawahi wateja wanapoingia dukani na kuwatamkia bei ya juu tofauti na bei halisi ili kile kinachozidi kiwe malipo yao.
“Mara nyingi bei za vitu sokoni zinapandishwa na mawinga bila sababu, ukitaka kupata bidhaa kwa bei halisi, hakikisha kwanza huyo unayezungumza naye ndiyo mmiliki wa duka vinginevyo utapigwa bei isiyo halali,” anasema.
Salum Mrisho, mfanyabiashara wa viatu wa Kariakoo, anashuhudia hali hiyo akisema mawinga hutafuta wateja na kuuza bidhaa kwa bei ghali zaidi ya uhalisia wakijipatia kipato zaidi ya mmiliki wa biashara hiyo.
“Mawinga wanatuletea wateja wengi sana na kusaidia kuuza bidhaa zetu haraka. Lakini wanapandisha bei mara nyingi na kuwa na wakati winga anaweza kupata pesa zaidi ya mmiliki wa bidhaa kutonana na anavyoelewana na mteja,” amesema.
Asha Mwenda, mfanyabiashara mwingine sokoni hapo, ameongeza kuwa gharama hizo huathiri biashara zao kwani baadhi ya wateja huona kama bidhaa zao zinauzwa bei ghali hasa winga akisimamia majadiliano ya bei hali inayofanya wateja kuondoka bila kununua bidhaa hata kama wamefikia bei halisi ya bidhaa hiyo.
Kwa upande wake, Rehema Mgonja, mkazi wa Kilungule Mbagala, amesema kupata fremu za biashara bila madalali ni vigumu, hali inayolazimu kutoa pesa za ziada kwa madalali ili wasaidie kuzungumza na wasimamizi wa fremu hizo.
“Nilikuwa natafuta fremu ya biashara hapa Kariakoo lakini nilichokutana nacho, madalali wanasema bila kutoa pesa hauwezi kupata fremu,” anasema.
Katika kukabiliana na hatua hiyo, Kampuni ya Masoko ya Karikaoo imesema imeandaa utaratibu maalumu ambao unawalinda wananchi wanaotafuta fremu dhidi ya utapeli wa madalali na mawinga wasio waaminifu kupitia mfumo wa kuomba fremu hizo mtandaoni.
Katika mfumo huo wa Serikali unaoitwa ‘Tausi’, mtu anatakiwa kujaza taarifa zake muhimu zikiwemo namba ya kitambulisho cha Taifa na namba ya mlipakodi (TIN) na kujaza taarifa muhimu tofauti na kuzungumza na mtu ana kwa ana kama wanavyodai kurubuniwa na madalali.
Mfumo huu unaondoa kabisa uwezekano wa mtu kati kujinufaisha na maeneo ya biashara kuwatoza fedha zisizo rasmi watu wanaohitaji fremu hizo.
Wawasifu mawinga, madalali
Mbali na malalamiko ya wengi, wapo pia wanaoeleza manufaa ya mawinga, wakitaja namna wanavyowezesha huduma kupatikana japo kwa gharama za ziada.
Dereva wa teksi mkazi wa Tabata, Hassan Mrope amesema bila madalali na mawinga kupata vyumba na bidhaa bora sokoni ni vigumu.
Amesema hawa wanajua maeneo muhimu ya kupata bidhaa, akibainisha kuwa wanasaidia kuokoa muda na kuepuka bidhaa za feki.
“Madalali na mawinga wanasaidia sana, wanaokoa muda kwani unaweza kumpa winga maelekezo tu akaenda sokoni, akatafuta na kukuletea bidhaa nyumbani kwako, ndipo ukafanya malipo, je, ungeenda mwenyewe ungetumia kiasi gani?” amesema.
Winga wa soko la Karume, Hamisi Jangala amesema uwinga siyo kazi ya uovu, huku akiomba wawekewe namna bora ya kufanya kazi hiyo inayowapatia kipato.
“Hii si kazi ya uovu, ni ajira, maana tunasaidia wananchi kupata bidhaa zenye ubora. Tunajua kona zote za masoko na hivyo tunasaidia jamii na familia zetu tunapopata riziki zetu,” amesema.
Abdul Mrope, dalali wa nyumba, mashamba na vyumba huko Tandika, Temeke, amesema madalali ni daraja muhimu wanaowezesha watu kupata huduma kirahisi tofauti na kama wangetafuta wenyewe mtaani, akisisitiza wajengewe namna bora ya kufanya kazi badala ya kuonekana watu wabaya na kuzuiwa kufanya kazi.
“Tunasaidia wananchi kupata vyumba wanavyotaka na kufanya makubaliano na wamiliki wa nyumba. Watu wengi hawawezi kuzunguka kutafuta huduma hizi bila msaada wetu.
“Hii kwetu fursa yetu ya kujipatia riziki na kusaidia watu kupata huduma,” amesema.
Mfanyabiashara wa Ilala, Fatma Abdallah, amekiri manufaa ya mawinga kuwaleta wateja na kuharakisha mauzo huku akifichua madalali hao wanavyopandisha bei ya bidhaa hizo.
“Wanasaidia sana katika kuleta wateja na kuuza bidhaa haraka, lakini ni kweli wanapopandisha bei,” amesema.
Kuhusu shughuli zao, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema haiwatambui mawinga na madalali, hivyo shughuli zao kwa sasa si rasmi na hazipo katika utaratibu wa kisheria, hali inayoonesha uhitaji wa hatua za haraka kuhusu mustakabali wa kundi hili.
Akizungumza na Mwananchi, leo Februari 9, 2026, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema mamlaka hiyo haimtambui mtu yeyote asiyekuwepo kwenye utaratibu rasmi wa kibiashara, hivyo madalali na mawinga si sehemu ya wajasiriamali wanaotambuliwa.
“TRA tunahusika na mfanyabiashara aliyesajiliwa, mwenye leseni na namba ya mlipakodi, tofauti na hapo, hao wengine hatuhusiki nao,” amesema.