DC Simanjiro ahimiza wanafunzi wote wapelekwe shule bila visingizio

Simanjiro. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Fakii Lulandana, amewaagiza wakuu wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha wanafunzi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza wanaanza shule mara moja bila visingizio.

Amesema baadhi ya wazazi wa jamii ya wafugaji hawatoi kipaumbele kwa elimu kwa kuwapeleka wavulana kuchunga mifugo na kuwaozesha wasichana wadogo baada ya kupokea mahari.

Akizungumza leo Februari 9, 2026 katika kikao cha tathmini ya matokeo ya upimaji wa kitaifa kilichofanyika Mirerani, amesema shule zote zimefunguliwa na hakuna mwanafunzi anayepaswa kubaki nyumbani.

DC Lulandana ameonya kuwa wazazi na walezi watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kukamatwa, huku dhamana yao ikiwa ni kuwapeleka watoto shule.

Pia amewahimiza walimu kujivunia taaluma ya ualimu na kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza ufaulu wilayani Simanjiro.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kaleiya Mollel, amewapongeza walimu kwa matokeo mazuri, huku Ofisa Elimu Awali na Msingi, Darius Limandola, akisema tathmini imelenga kuboresha ufaulu.