WADAU WA BIASHARA SHINYANGA WAPONGEZA JITIHADA ZA BARAZA LA USHINDANI

 

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Bw. David Lyamongi,akizungumza wakati wa semina ya kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya ushindani wa kibiashara wadau na wafanyabiashara wa mkoa wa Shinyanga iliyofanyika  katika Ukumbi wa Makindo, Shinyanga.

Na.Mwandishi Wetu-SHINYANGA

Baraza la Ushindani, kwa niaba ya Mwenyekiti wake, Mhe. Jaji Rose Ally Ebrahimu, limewashukuru wadau na wafanyabiashara wa Mkoa wa Shinyanga kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika semina ya kuwajengea uwezo iliyofanyika  katika Ukumbi wa Makindo, Shinyanga.

Semina hiyo imelenga kuwaongezea wadau uelewa kuhusu masuala ya ushindani wa kibiashara, haki zao kama wafanyabiashara pamoja na taratibu za kuwasilisha rufaa endapo hawataridhishwa na maamuzi ya mamlaka za udhibiti.

Akifungua semina hiyo, Bw. David Lyamongi, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salumu Hamduni, aliwataka wadau na wafanyabiashara kutumia vyema fursa hiyo ya kujifunza ili kuimarisha shughuli zao za kibiashara.

Aidha, aliishukuru Baraza la Ushindani kwa kuwaletea wakazi wa Shinyanga elimu muhimu inayolenga kulinda haki zao katika biashara na kuimarisha ushindani wa haki katika soko.

Akizungumza katika semina hiyo, Msajili wa Baraza la Ushindani, Mhe. Mbegu Kaskasi, alisema kuwa Baraza la Ushindani ni chombo cha Serikali kilichoanzishwa kwa lengo la kusikiliza na kutatua migogoro ya ushindani wa kibiashara. Alisisitiza kuwa Baraza linaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha wadau na wafanyabiashara wanalifahamu, kulifikia kwa urahisi na kulitumia ipasavyo wanapohitaji haki.

Kwa upande wake Mjasiriamali kutoka Mkoa wa Shinyanga , Bw. Dedani Rutazibwa,alipongeza Baraza la Ushindani kwa kuandaa semina hiyo ya kuwajengea uwezo wadau. Alisema kutokana na umuhimu wa chombo hicho, ameiomba Serikali kupitia Baraza la Ushindani kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika ngazi tofauti, ili wafanyabiashara waweze kufahamu haki zao pamoja na mamlaka sahihi za kuwasilisha rufaa zinazotokana na maamuzi ya mamlaka za udhibiti na Tume ya Ushindani.

Naye  Mkazi wa Shinyanga Mwl. Zezema Nyangaki, alisema kuwa elimu aliyopata kupitia semina hiyo imemfungua macho, akieleza kuwa awali hakuwa na uelewa kuhusu uwepo wa mamlaka za udhibiti zinazopokea malalamiko ya wafanyabiashara. Aliongeza kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kufahamu kuwa endapo hataridhishwa na maamuzi ya mamlaka hizo, anaweza kukata rufaa katika Baraza la Ushindani ili kupata haki yake kwa mujibu wa sheria.