:::::::::
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. CP Suzan Kaganda, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi pamoja na wanachama wa jumuiya za Watanzania wanaoishi katika maeneo ya Hwange na Bulawayo nchini Zimbabwe.
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi, yakiwemo ushiriki wao katika utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi pamoja na sera ya ubidhaishwaji wa lugha ya Kiswahili.
Katika mazungumzo hayo, Balozi CP Kaganda ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuhakikisha wanajisajili katika mfumo wa Diaspora Hub, akieleza kuwa usajili huo utawasaidia kuunganishwa na fursa mbalimbali za ajira, elimu, biashara na uwekezaji zilizopo katika maeneo ya uwakilishi. Aidha, usajili huo utasaidia pia katika utatuzi wa changamoto wanazokutana nazo katika maeneo yao ya makazi.


