Kocha Simba ataja chaguo jipya la Okello

MASHABIKI wa soka wa Yanga bado hawajui kilichoipata timu hiyo yenye nyota wakali na walioonekana huenda ikawa timu pekee ya Tanzania kutinga robo fainali kabla ya upepo kubadilika ghafla, lakini kuna kocha mmoja ameamua kufichua ‘code’ zinazoweza kuwabeba wananchi katika mechi ya mwisho ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie ya Algeria.

Kocha huyo aliyewahi kuinoa Simba na kuwahi kufanya kazi Uganda, amefichua kuwa, kama Yanga inataka kumfaidi zaidi Allan Okello iliyemsajili katika dirisha dogo, basi imtumie kama mshambuliaji wa pili (namba 10) na sio winga kama ilivyo sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa zamani wa Simba na Vipers ya Uganda alikotokea Okello, Mbrazili Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema Yanga imepata mchezaji mzuri, lakini amemwangalia katika mchezo uliopita ugenini dhidi ya FAR Rabat ya Morocco na kubaini hachezeshwi eneo zuri.

Robertinho amesema amewahi kukutana na Okello akiwa na timu nyingine kabla ya kutua Vipers iliyoiuzia Yanga nyota huyo hivi karibuni na alikuwa akimpasua kichwa kutokana na ubora alionao uwanjani.

“Okello wa sasa siye yule ninayemfahamu, kwani ana kiwango bora kuliko kile anachokionyesha Yanga kwa sasa, kwani nafasi anayocheza inaziba ubora alionao,” amesema Mbrazili huyo na kuongeza:

“Okello akichezeshwa namba 10 atakuwa hatari zaidi, kwani anabadilika kabisa akiwa eneo hilo anakuwa na nguvu ya kutoa pasi nyingi za  mabao (asisti), lakini pia ana uwezo wa kufunga kwa urahisi zaidi akiwa hapo.”

Robertinho alifafanua zaidi kwa kusema; “Anavyotumika sasa kama kiungo wa pembeni inampa changamoto kwa kuwa hana nguvu na kasi ya kumudu majukumu ya kucheza eneo hilo.

“Naamini Yanga imepata kiungo mzuri sana, kwa kuwa akibadilishiwa nafasi hata washambuliaji watafurahia zaidi kucheza naye kutokana na ubunifu wake. Wakati Okello akiwa KCCA na mimi naifundisha Vipers nilikuwa nikifanya kazi ngumu ya kuunda eneo la ulinzi na la kiungo ili kumdhibiti,” amesema Robertinho.

Okello alitua Yanga katika dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Vipers, timu iliyokuwa ikinolewa na Robertinho kabla ya hapo aliwahi kuichezea Kampala City ya Uganda na alikuwa kati ya mastaa waliopenya katika hesabu za kocha Pedro, licha ya kukuta mastaa wanaofanya vyema kikosini.

Hata hivyo, nyota huyo ameonekana kukosa makali kutokana na kupangwa eneo la pembeni kama winga na kama Yanga itaamua kutumia ushauri wa Robertinho, itakuwa na maana ya Pacome Zouzoua ampishe eneo la namba 10 ambalo pia lina wachezaji kama Mudathir Yahya.

Tangu atue Yanga, Okello amefanikiwa kucheza kikosi cha kwanza mara kadhaa huku akifikisha jumla ya dakika 339 katika mechi tano alizocheza, lakini hana bao lolote hadi sasa.