FAR Rabat watia mkono mechi ya Yanga

YANGA inapiga hesabu kwa sasa ni namna gani kikokotoo chake kitatoboa ili itinge robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini wale Waarabu wa Morocco wameibuka na kutia mkono mechi ijayo ya Zanzibar wakiwajaza upepo JS Kabylie ya Algeria kwamba wafanye kweli.

Wananchi watakuwa wenyeji wa JS Kabylie kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Siku ya Wapendanao, wakihitaji ushindi wa tofauti ya mabao mawili mbele ya Kabylie, iliyopoteza tumaini la kusonga mbele kupitia Kundi B linaloongozwa na Al Ahly ya Misri.

Wakati kocha Pedro Goncalves na vijana wa Jangwani wakipiga hesabu hizo na kuiombea mabaya FAR Rabat ya Morocco iliyo katika nafasi ya pili ipoteze ugenini Misri dhidi ya Al Ahly, wenyewe kupitia kocha wao, Alexandre Santos wametoa kauli ya kuwajaza upepo JS Kabylie visiwani.

Kocha Santos, raia wa Ureno aliliambia Mwanaspoti, licha ya kwamba JS Kabylie haina nafasi ya kufuzu, lakini ushindi dhidi ya Yanga utaipa heshima timu hiyo kutoka Algeria.

Santos amesema JS Kabylie ambayo haijashinda mechi yoyote ina nafasi ya kushinda Zanzibar na kubadilisha rekodi mbaya ya kumaliza mechi za makundi bila ushindi wowote ambayo itawafariji mashabiki wao.

“Tumecheza na JS Kabylie, kiukweli sio timu mbovu kabisa inacheza vizuri sana, haikuwa rahisi kutoka sare kwao na hata kuwafunga huku kwetu. Sidhani kama inastahili kumaliza mechi hizi bila kushinda hata mechi moja,” amesema Santos na kuongeza:

“Kabylie ina nafasi ya kushinda mchezo wa mwisho (dhidi ya Yanga) na kama wakifanya hivyo wanaweza kupanda hadi nafasi ya tatu. Hili likitimia itawafariji mashabiki wao. Ukienda kwenye uwanja wao unaona namna wanavyoipenda timu yao.”

Santos amesema anaipa hamasa JS Kabylie ishinde ili iwe rahisi kwa timu anayoinoa yenye pointi nane kwa sasa isonge mbele, kwani hata kama itapoteza Cairo, Misri, bado itaungana na Al Ahly kwenda robo fainali kutoka kundi hilo, na Yanga kusaliwa na pointi tano ilizovuna katika mechi tano.

Akiizungumzia FAR Rabat, Santos amesema haitakuwa mechi rahisi mbele ya Al Ahly, lakini watakwenda Misri kwa ajili ya kushinda.

“Tuna mechi ngumu. Tunafahamu kwamba Ahly imeshafuzu, lakini itahitaji kuongoza kundi. Tunatakiwa kujiandaa kwa ugumu huo. Hatutaki kupoteza kwani inaweza kuwapa nafasi Yanga ya Tanzania kushika nafasi ya pili, ni mchezo mgumu sana.”