Makapu, Bahanuzi waukubali mziki wa Bacca

MWENDELEZO wa kiwango anachokionyesha beki wa Yanga, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kimemuibua kiungo wa Bigman FC iliyopo Ligi ya Championship, Said Juma ‘Makapu’ anayeamini kinatokana na uvumilivu na nidhamu, huku straika mwingine wa kimataifa wa zamani, Said Bahanuzi akimpigia saluti.

Makapu aliyewahi kuichezea Yanga aliuelezea uchezaji wa Bacca kuwa ni wa kutumia nguvu, akili na kasi, kwamba unasaidia uimara wa safu ya ulinzi wa Wanajangwani. 

“Kwa nafasi ninayocheza ya kiungo mkabaji, tunapokutana na wapinzani nafahamu kabisa wachezaji wa kuwachunga, ndivyo ilivyo kwa Bacca anavyokuwa mwiba kwa timu inayokuwa inacheza na Yanga,” amesema Makapu na kuongeza;

“Nimecheza Yanga nafahamu ukiona mchezaji anategemewa kikosi cha kwanza, siyo kwa bahati mbaya ana bidii ya mazoezi, nidhamu ya kazi yake na kiwango kinakuwa na manufaa kwa timu,”

Hoja ya Makapu iliungwa mkono na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi aliyesema: “Bacca anatumia nguvu na akili kwa mshambuliaji hawezi kuingia kichwakichwa kwenda kuvaana naye, lazima ashambulie kwa akili kubwa.”