Dodoma. Ni mwaka wa sita sasa, Soko Kuu la Job Ndugai la jijini Dodoma bado halina watu, lakini waliopo wameendelea kupungua kila kukicha huku mitaa na barabara za ndani ya jiji zikifurika wafanyabiashara ndogondogo (machinga).
Hata hivyo, uongozi wa jiji unasema hawatatumia nguvu kupeleka wafanyabiashara huko, badala yake wanaboresha miundombinu ambayo itavuta kundi la watu ambao watakuwa ndiyo wateja wakubwa kwa wafanyabiashara.
Soko la Ndugai ambalo kabla lilijulikana kama Soko Kuu la Dodoma, limejengwa katika Kata ya Nzuguni na ujenzi wake uligharimu zaidi ya Sh14 bilioni ambapo lilianza kufanya kazi rasmi mapema mwaka 2020 likitaraji kuchukua idadi kubwa ya wafanyabiashara.
Hata hivyo, hali imekuwa ni kinyume na matarajio kwani wafanyabiashara wengi waliochukua vizimba na fremu za maduka walikimbia siku chache baadaye kwa kilichoelezwa kuwa hakuna wateja kwani limejengwa nje ya mji.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika soko hilo, Maulidi Ally, amesema hali ya biashara kwa sasa ni ngumu kwani wanaofanya biashara hapo wamepoteza mitaji yao na kujikuta wanakuwa na madeni kila mahali huku uendeshaji wa familia zao ukiwa mgumu.
Maulidi amesema ndani ya soko kuna vizimba zaidi ya 360 lakini waliopo kwa sasa hawazidi 45, wakati eneo la maduka makubwa lenye uwezo wa kuchukua zaidi ya wafanyabiashara 100 kwa sasa lipo wazi.
“Kwa kipindi cha miezi miwili nimekimbiwa na wafanyabiashara watano. Leo kwenye vizimba ni mavumbi na maturubai, watu hawauzi na wameamua kuhama hapa kwani wanazidi kufilisika na kuachiwa madeni, ila sheria za jiji wakati mwingine zinachangia haya yote,” amesema Maulidi.
Miongoni mwa sababu alizozitaja mfanyabiashara huyo ni kitendo cha jiji kuruhusu kila gari la mizigo kushusha maeneo ambayo hayaruhusiwi, akiyataja mfano wa eneo la Miti Mirefu na Dodoma Inn wakati Ndugai kuna eneo kubwa, hali ambayo inachangia kuwakimbiza wafanyabiashara.
Amekiri kuwa wengi wameamua kuhama hapo na kukimbilia mtaani baada ya masoko ya Majengo, Machinga na Sabasaba kuwa yamejaa na hakuna nafasi ya kuwapokea wengine.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kama uongozi ungetaka soko hilo likue basi wangefanya kama ilivyo kwa Soko la Machinga ambako walilazimisha magari yote kushusha na kupakia abiria hapo, lakini hali ni tofauti kwa Ndugai ambako wamechagua baadhi ya magari ndiyo yasimame hapo na mengine yanashusha na kupakia Dodoma mjini.
Akizungumzia soko hilo, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dk Frederick Sagamiko, amekiri kuwa soko hilo ni tupu lakini amesema ni muda mfupi watu watakimbilia huko wenyewe na hakutakuwa na nafasi ya kupata kwa urahisi kama wengi wanavyodhani.
“Jambo la msingi ni kwamba hatuwezi kuwapeleka wafanyabiashara kwa nguvu katika maeneo hayo. Jambo jema ni kuwatengenezea miundombinu mizuri itakayowapeleka kule, na hilo ndilo suluhisho, lakini siyo kukamata watu mitaani na kuwapeleka kule,” amesema Dk Sagamiko.
Mkurugenzi huyo amesema uongozi unatambua wingi wa machinga waliopo barabarani katikati ya jiji na tayari wameshaanza mchakato wa kujenga masoko mengine ya machinga katika eneo la Umonga na baadaye watajenga Kisasa ambako wanaamini kuna watu wengi watakaosababisha biashara zichangamke.
Amesema soko hilo lilijengwa kwa kuzingatia mipango miji ya siku za usoni ambako eneo hilo litakuwa na watu wengi na hakuna atakayehitaji kuingia katikati ya jiji.
“Kwanza Kata ile ndiyo ina watu wengi karibu 67,000, lakini tunapanua barabara kuu, soko lipo jirani na stendi ya mabasi ya mikoani, na kingine si mnaona watumishi wanajenga zaidi upande huo huku miji ya Ihumwa na Kikombo ikizidi kupanuka? Kwa hiyo tusitumie nguvu kuwapeleka, ila muda mfupi watakwenda wenyewe,” amesema.
Mfanyabiashara wa viatu katika Soko la Sabasaba, Godbless Chuwa, anataja sababu zilizomkimbiza Soko la Ndugai kuwa ni kukosekana kwa wateja wa kufanya biashara zao zichangamke, hali iliyopelekea kila wakati mtaji wake kuzidi kuchukua.
Chuwa anasema kati ya masoko ambayo yamejengwa vizuri na kuwa na miundombinu ya kisasa ni Soko la Ndugai, lakini kinachowakimbiza ni kwa sababu limejengwa pembezoni mwa jiji ambako hakuna muingiliano wa watu, licha ya kuwa hivi sasa mabasi yanayokwenda wilayani yanapakia na kushusha hapo kama kituo chao kikuu.
Mfanyabiashara huyo anaamini ujenzi wa uwanja wa mpira jirani na soko na upanuzi wa barabara kuu vitapeleka watu wengi katika Soko la Ndugai na hakutakuwa na mtu atakayekimbia wala kuondoa biashara zake kwani watu wengi watafurika eneo hilo, jambo ambalo anasema litachukua muda mfupi kuanzia sasa.