Wagonjwa 11 wa tezi dume watibiwa kwa teknolojia ya mvuke KCMC

Moshi. Wagonjwa 11 kati ya 56 waliobainika kuwa na tatizo la tezi dume katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) wamefanyiwa upasuaji kwa kutumia teknolojia mpya ya mvuke wa maji.

Upasuaji huo wa kitaalamu, unaotumia muda wa dakika 15 hadi 20, umefanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini katika hospitali hiyo, na unatajwa kuwa ni moja ya mafanikio makubwa katika sekta ya afya.

Akizungumzia mafanikio hayo leo Februari 10, 2026, Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Gabriel Chisseo, amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa madaktari bingwa wa hospitali hiyo pamoja na madaktari bingwa kutoka nchini India, ambao waliweka kambi ya siku sita kuanzia Januari 26 hadi 31 na kufanikisha upasuaji huo.

“Tulifanikiwa kuwaona wagonjwa 56 waliokuwa na changamoto ya tezi dume hapa hospitalini kwetu, na tuliweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 11 ambao kesho yake waliweza kuruhusiwa,” amesema Gabriel.

Amesema, “Moja ya sifa ya upasuaji huu wa njia ya mvuke ni kuwa na muda mfupi, na mgonjwa anakaa hospitalini kwa muda mfupi. Anaweza kufanyiwa leo na kutoka leo au kesho, inategemea mwili wake unavyokuwa baada ya kufanyiwa upasuaji.”

Aidha, amesema upasuaji huo uliofanyika hospitalini hapo umeonyesha mafanikio chanya na kwamba hakuna mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji na kubaki hospitalini hapo kwa zaidi ya siku moja.

“Hakuna mgonjwa aliyekaa hospitalini siku mbili. Zoezi lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa, na wote baada ya kufanyiwa upasuaji waliruhusiwa na wanaendelea vizuri na shughuli zao,” amesema Chisseo.

Aidha, amesema hospitali hiyo inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika teknolojia hiyo kwa kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana.

Akizungumzia teknolojia hiyo leo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Urolojia hospitalini hapo, Dk Frank Bright, amesema njia hiyo ya upasuaji ni salama na ina madhara pungufu kuliko njia ambayo ilikuwa ikitumika zamani, na kwamba damu haitoki nyingi kwa sababu hutumia mvuke.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Gileard Masenga amesema hospitali hiyo imelenga kutoa huduma bora kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, hususan Kanda ya Kaskazini.

Profesa Masenga amesema katika kitengo cha Urolojia, kwa siku wanaona wagonjwa 100 wenye matatizo mbalimbali ya mfumo wa mkojo, ikiwemo tezi dume.