Udhibiti bajaji, pikipiki za umeme ulivyo ‘kaa la moto’ kwa mamlaka-2

Dar/Dodoma. Hii ni sehemu ya pili ya janga linalochipuka linalohusisha bajaji na pikipiki zinazotumia nishati ya umeme, ambalo linaibua maswali kuhusu usalama barabarani na ugumu wa kuvitambua vyombo hivyo vinapohusika katika ajali.

Changamoto hiyo imeendelea kuwepo huku kukiwa na sintofahamu kuhusu nani hasa anapaswa kusimamia udhibiti wa kuhakikisha vyombo hivyo vinasajiliwa.

Sehemu hii inaangazia hali ya mamlaka husika kutupiana mpira kuhusu usimamizi wa bajaji na pikipiki za umeme, hususan katika kuhakikisha zinakidhi matakwa ya kisheria ikiwamo usajili, bima, na utambuzi wa namba za vyombo.

Moja ya changamoto ni kwamba bidhaa za pikipiki zinazotumia nishati ya umeme zilikuwa zikiingizwa nchini kama vipuri, kisha kuunganishwa na kuanza kutumika kibiashara bila kufuata taratibu za usajili.

Kiongozi wa Idara ya Sheria katika Idara ya Usalama Barabarani, Kamishna wa Polisi Mussa Manyama, anasema kuendesha gari lisilosajiliwa, iwe la mafuta au umeme, ni kinyume cha sheria na husababisha hatari kubwa za kiusalama.

Anasema, kama ilivyo kwa magari ya kawaida, kuendesha magari yanayotumia umeme bila kusajiliwa ni kosa linalostahili faini kubwa na kukamatwa kwa chombo husika, kwani hukosa bima na kuwaacha madereva, abiria, na watumiaji wengine katika mazingira magumu baada ya ajali.

Hata hivyo, hakutoa takwimu za kina kuhusu waliokamatwa au kuondolewa barabarani tangu tangazo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Tutaendelea kutekeleza sheria na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa usajili wa vyombo vya moto vinavyotumia dizeli, petroli au umeme,” anasema.

Meneja Usafirishaji Barabarani na Leseni wa Mamlaka ya Usafirishaji Ardhini (Latra), Patel Ngereza, anasema changamoto za usajili wa magari yanayotumia nishati ya umeme bado zipo, ingawa uelewa wa wananchi unaongezeka taratibu.

Anasema kati ya pikipiki zaidi ya 22,000 zilizosajiliwa Latra mwaka 2025, takribani asilimia nane zinatumia umeme.

Anaongeza kuwa licha ya jitihada za kuhamasisha usajili mwaka jana, mwitikio wa wadau haukuwa wa kuridhisha.

Ngereza anasema awali bidhaa za pikipiki zinazotumia umeme zilikuwa vinaingizwa nchini kama vipuri kisha huunganishwa na kuanza kutumika kibiashara.

“Hali hiyo ilitulazimu kuitisha vikao vya wadau kujadili umuhimu wa usajili na utoaji wa leseni za kibiashara,” anasema, akibainisha pia kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya taasisi yake na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika kushughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo ubora wa betri na vifaa.

“Pia, tulibadilisha kanuni zetu kuruhusu magari ya umeme kusajiliwa na kupewa leseni za kibiashara,” anasema, pasipo kutoa takwimu za utekelezaji, akisema lengo ni kuongeza elimu kwa umma.

Mkurugenzi wa Huduma kwa Walipa Kodi na Elimu wa TRA, Richard Kayombo, anasema magari yanayotumia nishati ya umeme yanafuata mfumo wa namba sawa na unaotumiwa na vyombo vinavyotumia diseli na petroli na kwamba wamiliki wanapaswa kuufuata na kulipa kodi za uingizaji kama wanavyohitajika.

Anasema Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani ndilo lenye mamlaka ya kuendesha operesheni dhidi ya magari yasiyosajiliwa.

“Wajibu wetu ni kutoa matangazo ya kuhamasisha usajili, lakini kukamata wanaokiuka sheria husika ni jukumu la polisi wa usalama barabarani,” anasema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, anasema wamiliki wa bajaji na pikipiki za umeme zinazoendeshwa bila kusajiliwa wanakiuka sheria.

Anaongeza kuwa wilaya inashirikiana na Jeshi la Polisi kukamata vyombo hivyo na kuhakikisha vinafuata sheria.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa umma na kushirikiana na watoa huduma za usafiri mtandaoni kukuza shughuli rasmi. Wakati wa ukaguzi, hatua za kisheria huchukuliwa dhidi ya madereva wanaobainika kuendesha vyombo hivyo bila usajili, ikiwemo faini,” anasema.

Shirika la haki za abiria

Mkurugenzi wa Shirika la Kupigania Haki za Abiria Nchini (Shikuhata), Ambakise Mwakifwange, anasema usafiri unaotumia vyombo visivyosajiliwa unadhoofisha usalama, uwajibikaji, na imani ya umma.

Anasema bila usajili, ajali haziwezi kufuatiliwa, kesi haziwezi kuendeshwa ipasavyo, na fidia haiwezi kutolewa kwa haki.

Anaitaka Serikali kufanya ukaguzi maalumu, kutoa elimu kwa madereva na abiria, na kutunga kanuni mahsusi kwa usafiri wa vyombo vinavyotumia umeme, akisema: “Abiria wanapaswa kukataa kupanda vyombo visivyosajiliwa na visivyo na sahani ya namba.”

Kuhusu bima, Mkurugenzi wa Utekelezaji na Huduma za Uthaminishaji wa Mamlaka ya Huduma za Bima Tanzania (TIRA), Alex Rocky, anasema awali kulikuwa na changamoto kutoa bima kwa magarai yasiyo na usajili.

Anasema baada ya tangazo la TRA Mei 15, 2025, magari yanayotumia nishati ya umeme yameanza kusajiliwa na kupewa bima kama mengine, akisisitiza: “Fidia haitolewi kwa magari yasiyo na bima halali.”

“Magari yasiyo na usajili au bima huwaacha wahanga bila haki za kisheria, yanaongeza umaskini na kuathiri ustawi wa jamii. Kila chombo cha moto kinachotembea barabarani kinapaswa kuwa na bima,” anaongeza.

Anasema Tira inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya vyombo vya umeme, ikiwemo usajili na bima, kupitia kampeni za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

“Hii pia ni fursa kwa kampuni za bima kubuni bidhaa maalumu kwa magari yanayotumia nishati ya umeme, ikizingatiwa faida zake kimazingira na ongezeko la mahitaji,” anasema.

Anasema sheria ipo wazi, lakini utekelezaji unachelewa, akizitaka mamlaka kuimarisha ukaguzi, utoaji wa elimu, na utekelezaji wake ili kuhakikisha ukuaji wa sekta ya usafiri kwa kutumia magari yanayotumia nishati ya umeme pasipo kuhatarisha usalama, kukuza uwajibikaji, na kuchochea ukusanyaji sahihi wa mapato ya Serikali.

Mwanachama wa Tanzania Electric Mobility Association (Taema), Tony Mlela, anasema kabla ya kutungwa kwa sheria, baadhi ya bajaji na pikipiki zinazotumia nishati ya umeme zilikuwa zikiendeshwa bila kusajiliwa.

Anasema taratibu zinaendelea kurekebisha dosari mbalimbali na kuonya kuwa ni hatari kuruhusu magari kuwa barabarani bila kusajiliwa. Anabainisha kuwa utekelezaji bado unakabiliwa na changamoto, hasa kwa kampuni za usambazaji zinazokabiliwa na ucheleweshaji wa taratibu.

Hata hivyo, anasema baadhi ya vyombo tayari vimeshasajiliwa, huku bajaji nyingi za umeme zikikamilisha usajili wake.

Kuhusu kanuni na sera, Mlela anasema chama chake kimewasilisha mapendekezo yanayolenga ukuaji endelevu wa sekta hiyo, kikizingatia uzoefu wa Rwanda, Kenya, Uganda, na Ethiopia, ambazo tayari zina sera madhubuti za usafiri wa vyombo vinavyotumia nishati ya umeme.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa idadi kubwa ya bajaji na pikipiki hizo zinazofanya shughuli zake katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma zinaendeshwa bila kusajiliwa, bila kuwa na bima, na bila kubandikwa namba za usajili, hali inayokiuka matakwa ya kisheria.

“Ni vigumu kumfuatilia dereva ambaye bajaji au pikipiki yake imehusika katika ajali au uhalifu kwa sababu mara nyingi hukimbia baada ya tukio,” anasema mfanyabiashara wa Kariakoo, Mussa Kinabo.

“Bajaji na pikipiki zisizosajiliwa huongeza ukubwa wa tatizo kwa sababu ya ugumu wa kuwakamata na kuwachukulia hatua, hasa kwa sababu pia ya kukosekana kwa ushahidi wa utambulisho wa chombo kilichohusika na tukio,” anaongeza.

Mfanyabiashara wa jijini Dodoma, Happy Silvano, anasema mahitaji ya usafiri yanaongezeka kwa kasi, jambo linalowalazimu baadhi ya wamiliki kuendesha vyombo hivyo bila kusajiliwa.

“Sijawahi kusikia dereva ametozwa faini, jambo linaloonesha changamoto kubwa katika utekelezaji wa sheria za usalama barabarani, licha ya kuwa tunafanya nao kazi kila siku,” anasema.

Wananchi wanasema licha ya vyombo hivyo vinavyotumia umeme kuwa nafuu, kuendesha bila usajili kunazidisha hatari ya ajali, uhalifu, na upotevu wa mapato ya Serikali kutokana na kutokusanywa kwa faini na adhabu za usajili.

“Bajaji na pikipiki nyingi hupata ajali na kuwaacha watu wengi na ulemavu wa kudumu, hasa kutokana na ongezeko la ajali na vitendo vya uhalifu katika majiji haya,” anasema mkazi wa Dar es Salaam, Simon Lunda.

“Kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri wa haraka kunachochea uhalifu na uporaji. Wengine hunyang’anya simu na vitu vya thamani wanapokuwa barabarani, abiria wanaotumia usafiri wa umma na madereva wa magari binafsi hasa vyombo vyao vinapokuwa kwenye foleni,” anasema mkazi wa Dodoma, Linda Kisasa, na kuongeza kuwa baada ya kutekeleza uhalifu hutokomea haraka.

Dereva wa daladala jijini Dar es Salaam, Hamisi Doto, anasema gari yake iliwahi kugongwa na bajaji inayotumia umeme na kwamba baada ya kubaini haikusajiliwa na haikupata madhara makubwa, aliamua kuendelea na safari.

“Kama ingekuwa gari au pikipiki iliyosajiliwa, tungezungumza na baadaye ningelipwa fidia,” anasema, na kuhoji kiasi cha mapato ambacho Serikali inapoteza kwa kutokusanya faini na adhabu za usajili.

Mfanyabiashara wa eneo la Jamhuri jijini Dodoma, Rita Massawe, anasema bajaji na pikipiki za umeme hazitoi kelele kama zile zinazotumia dizeli na petroli.

“Siku moja nilikaribia kugongwa kwa sababu zilifika kimya kimya mahali nilipokuwa nimesimama,” anasema, akiongeza kuwa mara nyingi wanapohusika na ajali au uhalifu hukimbia toka eneo la tukio.