Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kisha kuiba Klabu ya The Voice Tz Limited, inayowakabili Tumaini Moshi (33) na Gasper Mmari (24), umekamilika.
Tumaini na Mmari ambao wote ni wakazi wa Kinyerezi wilaya ya Ilala, wanakabiliwa na shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha na kujipatia vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh1.5 bilioni mali ya klabu hiyo.
Kutokana na kukamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga kesho Jumatano Februari 11, 2026, Jamhuri kuwasomewa hoja za awali washtakiwa hao na kisha ianze kusikilizwa ushahidi.
Wakili wa Serikali, Eva Kassa ameieleza Mahakama hiyo, leo Jumanne Februari 10, 2026 wakati kesi hiyo ilipotajwa.
“Upelelezi wa kesi hii umekamilika na shauri hili limeitwa leo kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hoja za awali, lakini kwa bahati mbaya bado hazijawa tayari, hivyo tunaomba ahirisho fupi ili tuweze kukamilisha” ameomba Wakili Kassa.
Kassa ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.
Baada ya Jamhuri kutoa taarifa hiyo, Hakimu Swallo aliwaeleza washtakiwa hao kuwa kesi hiyo imehamishiwa kwake na imepangwa kusikilizwa ndani ya mwezi mmoja ili iwe imeisha.
“Washtakiwa kesi yenu imehamishiwa kwangu na maelekezo niliyopewa ni kwamba kesi hii inatakiwa ndani ya mwezi mmoja iwe imeshasikilizwa ushahidi na kutolewa uamuzi, hivyo kesho baada kusomwa Ph, tutaipangia tarehe kwa ajili ya kusikiliza mfululizo,” amesema hakimu Swallo na kisha kuiahirisha hadi kesho
Awali, kesi hiyo ya jinai namba 28915 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha, ilikuwa inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki, lakini kwa sasa itakuwa mbele ya Hakimu Swallo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa Oktoba 29, 2025 eneo la Kinyerezi katika Klabu ya The Voice Tz Limited, walifanya unyang’anyi wa kutumia silaha na kisha kuiba vitu vilivyokuwepo katika klabu hiyo.
Alidai kuwa siku hiyo ya tukio, Moshi na Mmari wanadaiwa kuiba viti 350 vya mbao na vya plastiki vikiwa na thamani ya Sh150 milioni.
Pia wanadaiwa kuiba vifaa vya ofisi vikiwa na thamani ya Sh40 milioni.
Iliendelea kudaiwa kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kuiba luninga 57, zikiwa na thamani ya Sh480 milioni.
Pia wanadaiwa kuiba Music System wenye thamani ya Sh250 milioni na POS mashine ikiwa na thamani ya Sh80 milioni.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba vyombo vya jikoni vyenye thamani ya Sh25 milioni
Vile vile, washtakiwa hao wanadaiwa kuiba vifaa vya baa yenye thamani ya Sh15 milioni.
Pia wanadaiwa kuiba vinywaji mbalimbali vyenye thamani ya Sh518 milioni.
Mbali na kuiba vitu hivyo, washtakiwa hao wanadaiwa kuiba fedha taslimu Sh16.9 milioni.
Jamhuri iliieleza Mahakama kuwa jumla ya vitu vilivyoibiwa vina thamani ya Sh1.5 bilioni, mali ya Klabu ya The Voice Tz Limited.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walisomewa shtaka hilo Desemba 10, 2026 na kupelekwa rumande kutoka na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.