Prisons hali tete, Coastal yafanya kweli

Wakati Coastal Union ikifufuka Ligi Kuu Bara, Tanzania Prisons hali imezidi kuwa mbaya baada ya kukosa ushindi kwa mchezo wa nane mfululizo na kubaki kwenye presha ya kurudi Championship msimu ujao. 

Coastal Union imefufuka leo baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa  leo, Februari 10, 2026, katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. 

Kabla ya ushindi huo, Wagosi hao walisota kwa michezo saba bila kuonja pointi tatu na matokeo hayo yanawafanya kupanda hadi nafasi ya tisa wakiwa na pointi 14 baada ya mechi 14.

Prisons wanafikisha michezo minane mfululizo bila kuonja pointi tatu na kubaki nafasi mbili za mkiani wakiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi 12. 

Katika mchezo huo ambao umepigwa saa 8 mchana, Coastal Union ilianza kucheka na nyavu dakika ya pili kupitia kwa Bakari Msimu kabla ya Shiza Kichuya kuongeza la pili, huku dakika ya 45 George Mpole akiipatia Prisons bao la kujifariji. 

Kipindi cha pili Prisons waliendelea kusota kwa kuruhusu tena wavu wao, ambapo dakika ya 85 Msimu aliiingia tena wavuni kabla ya Cleophas Mkandala kuhitimisha karamu ya mabao na kuihakikishia pointi tatu Coastal Union. 

Kocha Mkuu wa Coastal Union, Mohamed Muya amesema ushindi huo ni shukrani kwa mashabiki na viongozi wa timu hiyo kwa kuwavumilia muda mrefu baada ya kusota na matokeo yasiyo ridhisha. 

Amesema wamekuwa katika kipindi kigumu haswa baada ya baadhi ya mastaa kukumbwa na majeraha na kufanya benchi la ufundi kuhaha na muunganiko hivyo ushindi wa leo unawapa nguvu, hamasa na matumaini ya kuendelea kufanya vizuri. 

“Ushindi huu ni shukrani sana kwa uongozi na mashabiki kwa kutuvumilia kwa matokeo tuliyopitia, haikuwa kazi ndogo kwa kuwa kuna mambo yalitokea ni vile hatutangazi kila kitu, ilitufanya kutengeneza muunganiko kikosini,” amesema Muya. 

Kocha msaidizi wa Prisons, Innocent Mwamgonde amesema kiu na malengo yao ilikuwa ni kushinda mechi hiyo, lakini kukosa umakini kwa nyota wao ndio iliwapa wakati mgumu dhidi ya wapinzani hao. 

Amesema licha ya matokeo hayo, lakini hawajakata tamaa akitoa matumaini kuwa mzunguko wa pili watabadili upepo na kupata matokeo mazuri.

“Wachezaji wamekosa umakini wenyewe ila bado tunayo nafasi kwakuwa Ligi haijaisha, mzunguko wa pili tunaweza kurudi kivingine, hatujakata tamaa, tutasahihisha makosa,” amesema Mwamgonde.