Dar es Salaam. Wafanyabiashara katika soko la nyama choma Vingunguti, maarufu Soko la Kumbilamoto wameanza mgomo wa biashara wakilalamikia kodi kubwa na tozo nyingi wanazodaiwa kulipa kila mwezi.
Leo Februari 10, 2026 wafanyabiashara wa soko hilo wamegoma kufungua biashara wakisema hali hiyo imekuwa kero na unyanyasaji unaowafanya washindwe kuendesha maisha yao.
Soko hilo lilizinduliwa rasmi Mei 24, 2025 ikiwa ni hatua ya Serikali kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo na kuongeza usalama, usafi na mpangilio katika shughuli za uuzaji wa nyama na chakula jijini Dar es Salaam.
Wafanyabiashara hao wamelalamika kwa kulipa kodi ya Sh10,000 kwa wenye maduka, Sh30,000 mama lishe na wachoma nyama na wao wanalipa Sh60,000 mbali na gharama za usafi, umeme na maji.
Wamedai kuwa malipo hayo yanapokelewa mara mbili kwa wanaoingia mchana na usiku hivyo waliomba kupunguziwa gharama ili wamudu kujiendesha.
Akizungumza na Mwananchi, mama lishe wa soko hilo, Ashura Kilambwe amesema amepiga hesabu na kubaini anatakiwa kulipa Sh65,000 kila mwezi.
Amesema kutokana na hali ya biashara wamekuwa wakiomba walipe kila siku ili isiwaumize hata inapotokea hajafika eneo la biashara inampunguzia gharama.
“Tumeshaomba sana jambo hili na kushirikiana na wenzangu tukaandika hadi barua kuomba hili jambo la kodi lifanyiwe kazi kwani hali ya biashara sio nzuri, na ikiwezekana tulipe kwa siku kama ilivyo kwenye masoko mengine lakini tulikatalia,” amesema Ashura.
Amesema asilimia kubwa wanaofanya biashara eneo hilo ni watu wanaojitafuta hivyo ni ngumu kumudu kutoa pesa kwa mkupua kama wanavyohitajika hususan kwa mama lishe.
“Nina watoto na wajukuu ninaowalea, wazazi wao wamefariki, kila siku mtoto anakuja kuniomba hela ya daftari na ya chakula shuleni. Lakini biashara yenyewe inakufa kwa sababu ya kodi kubwa,”amesema.
Naye, mchoma nyama wa eneo hilo, Khamis Kisonge amesema kwa upande wao yapo majiko zaidi ya 60 wameomba kupunguziwa gharama, lakini imeshindikana kwani kuna huduma nyingine zimekuwa ni shida hivyo wanatumia vitu vya ziada.
Amesema malipo yao ni Sh60,000 kwa kila mwezi pamoja na gharama za taa ambazo hulipiwa Sh2,000 kwa siku kwa wafanyabiashara wanaofanya kazi usiku, hali inayoongeza mzigo wa kifedha.
“Tumeomba kupunguziwa kodi zaidi ya mara 10, lakini hakuna anayetusikiliza, tumechoka sasa tumelazimika kufanya mgomo ili kilio chetu kifike kwa viongozi wa juu,” amesema Kisonge.
Wafanyabiashara hao pia wamelalamikia tabia ya kukamatwa meza au bidhaa endapo mtu atachelewa kulipa kodi hata kwa mwezi mmoja, wakisema hawaruhusiwi kulipa kidogokidogo bali hulazimika kulipa fedha yote kwa mkupuo.
“Kama hukulipa mwezi mmoja, wanakuja wanachukua meza, huu ni unyanyasaji. Tunajiuliza, hili soko ni la Serikali au la mtu binafsi? Kama ni la Serikali, kwa nini kodi ni kubwa kiasi hiki?” amehoji mfanyabiashara Mariam Msigwi.
Amesema masoko mengi ya Serikali hutoza ushuru wa kila siku kulingana na mauzo ya mfanyabiashara, lakini katika soko lao wanatakiwa kulipa kodi ya mwezi mzima bila kuzingatia hali ya biashara.
Kwa pamoja, wafanyabiashara hao wameiomba Serikali, viongozi wa halmashauri na mamlaka husika kuingilia kati, kupunguza kodi na kuweka mfumo rafiki unaolinda wajasiriamali wadogo waliolengwa kunufaika na soko hilo.
Akizungumza na Mwananchi, Meya wa jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal, maarufu Shetta amesema atafanyia kazi jambo hilo kwani hana taarifa nalo.
“Nimesikia na nitafanyia kazi taarifa hizo kwa sababu sina na taarifa yoyote,”amesema Shetta.